TRA yawekeza mil 37/- elimu ya kodi Tosamaganga

WANAFUNZI 270 wa Shule ya Sekondari Tosamaganga mkoani Iringa wanatarajia kunufaika na maboresho ya mazingira ya kujifunzia na kupata elimu ya kodi baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukabidhi vifaa vya TEHAMA vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 37 kwa klabu ya kodi shuleni hapo.
Vifaa vilivyokabidhiwa Oktoba 30, mwaka huu ni pamoja na kompyuta 20, printer moja, mashine ya fotokopi, fulana 270 pamoja na vitabu na machapisho mbalimbali kuhusu elimu ya kodi.
Hatua hiyo inalenga kuwaandaa vijana kuelewa umuhimu wa kodi na kujenga utamaduni wa ulipaji kodi kwa hiari kabla ya kuingia katika maisha ya utu uzima na shughuli za kiuchumi.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo, Meneja wa TRA Mkoa wa Iringa, Mai Gloria Saria, alisema msaada huo ni sehemu ya kutekeleza ahadi iliyotolewa na mamlaka hiyo wakati wa maadhimisho ya miaka 100 ya shule hiyo.
Alisema TRA imeamua kuwekeza katika elimu ya kodi kwa vijana tangu wakiwa shuleni ili wakue wakiwa na uelewa wa wajibu wao kwa taifa na umuhimu wa kuchangia maendeleo kupitia kodi.
Aliongeza kuwa vifaa hivyo vitawasaidia wanafunzi kutumia teknolojia katika kufanya tafiti, kukuza ubunifu na kupata taarifa sahihi kuhusu masuala ya kodi na maendeleo ya taifa.

Saria aliwataka wanachama wa klabu hiyo kuvitumia vizuri vifaa hivyo na kuwa mabalozi wa elimu ya kodi kwa wanafunzi wenzao na jamii inayowazunguka, hususan kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari, kudai na kutoa risiti.
Alisisitiza kuwa kodi ni sehemu ya uzalendo kwa kuwa mapato yanayokusanywa na Serikali husaidia kugharamia huduma za kijamii zikiwemo elimu, afya, barabara na miundombinu mingine ya maendeleo.
Kwa upande wake, Meneja wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa TRA ambaye pia ni msimamizi wa Klabu za Kodi nchini, Hudson Kamoga, alisema msaada huo ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha klabu za kodi katika shule mbalimbali nchini.
Alisema lengo ni kujenga kizazi kitakacholipa kodi si kwa sababu ya kufuatiliwa na mamlaka, bali kwa kutambua umuhimu wake na kuona kutimiza wajibu huo kama sehemu ya uzalendo.

Kamoga alisema elimu hiyo inapaswa kuanza mapema ili vijana waelewe kuwa kila anayepata kipato ana wajibu wa kuchangia maendeleo ya taifa kupitia kodi.
Akizungumzia maendeleo ya klabu hiyo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Tosamaganga, Laurent Manga, alisema klabu hiyo ilianzishwa mwaka 2025 na kwa sasa ina wanachama 270.
Alisema tangu kuanzishwa kwake imekuwa ikiimarisha uelewa wa wanafunzi kuhusu wajibu wa kulipa kodi kwa hiari, namna mapato ya Serikali yanavyokusanywa na mchango wake katika kukuza uchumi.
Manga aliishukuru TRA kwa kuendelea kushirikiana na shule hiyo, akisema vifaa vilivyotolewa vitaongeza ari ya wanafunzi kushiriki shughuli za klabu na kuboresha upatikanaji wa maarifa.
Alisema awali shule ilikuwa na baadhi ya vifaa vya TEHAMA, lakini havikutosheleza mahitaji yaliyopo, hivyo ongezeko hilo litasaidia kurahisisha ujifunzaji na upatikanaji wa taarifa.
Naye Joshua Msafiri, kutoka uongozi wa shule hiyo, alisema vifaa hivyo vitaunga mkono azma ya shule ya kuimarisha matumizi ya teknolojia katika ufundishaji na ujifunzaji, ikiwemo kufanya tafiti na kuongeza ufanisi wa kitaaluma.
Kwa upande wake, mwanafunzi na mwanachama wa Klabu ya Kodi, Godfrey Mbonde, alisema vifaa hivyo vitawapa fursa ya kupata maarifa zaidi kuhusu kodi na kuelewa namna inavyochangia kuboresha maisha ya wananchi.
Alisema kupitia klabu hiyo wamekuwa wakijifunza wajibu wa raia katika ulipaji kodi na matumizi ya mapato ya Serikali katika kutekeleza miradi ya maendeleo.



