TRC waagizwa kuongeza huduma za kisasa SGR

DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amelitaka Shirika la Reli Tanzania (TRC), kuongeza huduma mbalimbali kama huduma za kifedha katika jengo la stesheni la SGR ili kukidhi mahitaji kwa wasafiri.

Prof Mbarawa ametoa maelekezo hayo leo Februari 11, 2025 alipozidua huduma ya Mgahawa wa KFC iliyofunguliwa ndani ya stesheni hiyo, huku akimpa kongole mmiliki wa mgahawa huo kwa uwekezaji huo na kumsihi afungue huduma hiyo katika Mkoa wa Dodoma na Morogoro.

Amesema kuwepo kwa KFC katika katika jengo la SGR kutaimarisha shughuli za kiuchumi kutokana na bidhaa zote zinazotumika zinatoka Tanzania na pia kutoa ajira na fursa ya kujenga ujuzi kwa vijana wa kitanzania.

Advertisement

“Hapa Dar es Salaam KFC imetoa fursa mpya za ajira kwa watanzania hasa kwa vijana, nimejulishwa kuwa kampuni hii inaajiri na kutoa mafunzo kwa vijana zaidi ya 800, ikiwepo kuwapa ujuzi muhimu katika ukarimu, huduma ya chakula, usala wa chakula na usimamizi bora wa chakula. Hivyo wasafiri sasa wanahadhi ya kupata chakula chenye hadhi ya kimataifa na chenye Ladha bora,” amesema Prof Mbarawa.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya Ilala Edward Mpogolo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli la SGR, Masanja Kadogosa kwa kutoa nafasi kwa wawekezaji kwa kuwa inachangia kukuza uchumi wa nchi.

“Tunamshukuru Mtendaji Mkuu wa SGR Kadogosa kwa kuwa mwepesi na mchangamfu wa kuwapokea wawekezaji kwa hali ya kawaida angekuwa mtu mwingine angesema haya mambo ya kupikapika ndani ya jengo langu mimi ‘hapana’ lakini amekuwa mwepesi na akatoa ushirikiano mkubwa,” amesema DC Mpogolo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Masanja Kadogosa amesema, kuwa na uwekezaji huo katika mradi wa SGR ni heshima kubwa kwa kuwa huwezi kuikuta kila mahali.

Mkurugenzi Mkuu wa Dough Works Limited, Vikram Desai, amesema mgahawa huo mpya ulioanzishwa chini ya Dough Works umechangia ajira za ndani, umetoa mafunzo, ukuzaji wa taaluma, fursa na kuimarisha nguvu kazi ya Tanzania na kukuza uchumi kwa ujumla.

tunajivunia kuwa sehemu ya safari hii kwa kuleta chapa hii maarufu duniani kwa wasafiri nchini Tanzania, pia tunatengeneza nafasi za kazi, tunawezesha jamii na kuchangia ukuaji wa uchumi” amesema Desai.

 

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *