TRC yaongeza safari treni mikoa mitatu

SHIRIKA la Reli Tanzania-TRC-limetangaza kuongeza safari za treni kwenda mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka.

Taarifa ya TRC iliyotolewa leo imesema siku ya Jumatano itaongezeka kujumuisha siku za Jumatatu na Ijumaa hivyo kufanya jumla ya safari tatu kwa juma kuelekea mikoa hiyo.

Imesema ongezeko hilo la siku ya Jumatano ni hatua mahususi za TRC kukabiliana na ongezeko la abiria katika kipindi hiki hususani kuelekea mikoa ya Kaskazini Mashariki mwa Tanzania.

Advertisement

Katika hatua nyingine kila siku ya Jumatatu ya juma kuanzia Desemba 09, 2024 mpaka mwanzoni wa Januari 2025 Shirika litakuwa likipeleka mabehewa 18 yatakayobeba abiria takribani kati ya 1,000 na 1,200 kwa wakati mmoja kuelekea mikoa hiyo.

Taarifa imesema TRC inawahakikishia wananchi kwamba hakutakuwa na ongezeko la nauli katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka hivyo nauli zitasalia kama zilivyo sasa.

Nauli ya shilingi 16,500 daraja la tatu, shilingi 23,000 daraja la pili kukaa na shilingi 39,100 daraja la pili kulala kwenda Moshi, zitasalia hivyo.

Aidha, nauli ya shilingi 18,700 daraja la tatu, shilingi 26,700 daraja la pili kukaa na shilingi 44,400 daraja la pili kulala kwenda Arusha, zitasalia hivyo.