Trilioni 455/- zahitajika malengo Dira 2050

SERIKALI imesema Tanzania inahitaji kuvutia Dola za Marekani bilioni 185 (Sh trilioni 455) katika kipindi cha miaka mitano ijayo ili ifikie malengo makuu ya Dira 2050.

Malengo hayo ni katika kipindi cha kati ikiwa ni pamoja na kujenga nchi ya viwanda, miundombinu fungamanishi na biashara imara.

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amesema hayo wakati akifungua jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Marekani lililofanyika kando ya kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA 80) jijini New York nchini Marekani.

SOMA: Mpango asisitiza amani Umoja wa Mataifa

Dk Mpango amesema fedha hizo kwa miaka mitano ni sawa na Dola za Marekani bilioni 37 (Sh trilioni 91) kila mwaka.

Amesema Serikali ya Tanzania inatambua sekta binafsi ni mshirika mkuu katika juhudi za maendeleo kwa ajili ya mabadiliko ya kijamii na kiuchumi hivyo inaboresha na kuweka mazingira wezeshi kwa biashara na uwekezaji.

Dk Mpango amesema Tanzania imekuwa na utulivu wa kisiasa na kijamii kwa miaka 60, mazingira ya biashara na miundombinu vimeboreshwa, hivyo wafanyabiashara na wawekezaji wa Marekani wanaweza kutumia fursa
hiyo kuwekeza.

Amesema serikali imepunguza muda wa usajili wa biashara kutoka siku 14 hadi saa 24, vibali vya uwekezaji vilivyokuwa vikichukua miezi, sasa vinachukua saa au siku kupitia Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (TISEZA).

Ataja fursa za uwekezaji

Uwekezaji wa mitaji wa moja kwa moja kwa mwaka kutoka Marekani uliongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 12.3 mwaka 2020 hadi Dola za Marekani milioni 40 mwaka 2023, huku uwekezaji wa jumla wa mitaji ukifikia Dola za Marekani bilioni moja.

Biashara ya bidhaa baina ya Tanzania na Marekani kwa jumla imeongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 228 mwaka 2020 hadi Dola za Marekani milioni 770 mwaka 2024.

Mwaka jana Marekani iliuza Tanznia bidhaa za Dola milioni 566 na mauzo ya Tanzania kwenda Marekani yaliongezeka kutoka Dola milioni 47 mwaka 2020 hadi Dola milioni 204 mwaka 2024.

Dk Mpango amewakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Marekani kuwekeza nchini Tanzania katika sekta za kimkakati yakiwemo madini adimu ya kinywe yaliyopo Mahenge mkoani Morogoro.

Aidha, ametaja fursa zilizopo Tanzania katika sekta ya kidijiti na akasema mabadiliko ya kidijiti ambayo yamefanyika nchini Tanzania ni dalili ya uwezo mkubwa uliopo.

Dk Mpango amesema Tanzania inahitaji washirika katika kilimo janja, teknolojia ya ndege zisizo na rubani, kilimo kinachoendeshwa na akili unde na uwekezaji katika maeneo ya usindikaji wa mazao ya kilimo.

Ametaja kuna fursa katika huduma za afya kama vile kushirikiana na kampuni za Marekani katika kutengeneza dawa na vifaatiba kwa ajili ya watu wa Afrika Mashariki wapatao milioni 300 na watu bilioni 1.4 katika Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA).

Dk Mpango amesema pia kuna fursa katika sekta ya miundombinu amesema Reli ya Kisasa (SGR) yenye urefu wa kilometa 2,561 itabeba abiria na tani 10,000 za mizigo kwa kila treni ikiunganisha Uganda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Rwanda.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button