DAR ES SALAAM; KAMPUNI ya Magazeti ya Serikali (TSN) inatarajia kuandaa toleo la kwanza la Jarida la ‘Mwangwi wa Ukarimu’ (Echoes of Kindness) linaloandaliwa na Daily News Digital.
Akizungumza leo Oktoba 19, 2023 Mratibu wa Jarida hilo na Kaimu Meneja wa Huduma za Habari za Kidijitali, Sylivester Domasa amesema lengo ni kusherehekea vitendo vya kipekee vya ukarimu na huruma vinavyoainisha Tanzania mwaka 2023.
“Tunaamini katika nguvu ya kutambua mashujaa wetu wa ndani katika makundi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na afya, elimu, mazingira, michezo, siasa, na mengine mengi, ”amesema Domasa na kuhoji:
“Je, wewe ni mmoja wa mashujaa hawa, au unamjua mtu anayestahili kutambuliwa? Ikiwa jibu lako ni ‘NDIYO,’ tunakualika kuwa sehemu ya safari hii yakufurahisha.
“Tutumie hadithi zako za wema au pendekeza mtu aliyeleta athari chanya, kwenye kurasa za jarida letu, tutaonesha ukarimu wa kipekee unaoenea katika jamii zetu na kukuza ‘Mwangwi wa Ukarimu’ unaochochea mabadiliko chanya,”amesema.
Aidha ameiomba jamii kujiunga na TSN linapoundwa jukwaa hilo, ambapo wema unang’aa na mashujaa wanasherehekewa.
“Tuungane kwa pamoja tuhamasishe, tutulize, na tuchochee mabadiliko Tanzania. Hadithi zako ni moyo wa ‘Vipande vya Ukarimu,’ na pamoja, tutafanya wema kuwa moyo wa taifa letu,” amesema.
Ametaja makundi yatakayofikiwa ni Maendeleo ya Jamii, Elimu na Kuwezesha Vijana, Shujaa wa Huduma za Afya, Uhifadhi wa Mazingira, Msaada wa Kibinadamu, Ubunifu na Teknolojia, Uhifadhi wa Utamaduni na Sanaa.
Mengine ni Msamaria Mwema – Mtu Mzima, Msamalia Mwema – Kijana, Viongozi Vijana wenye Kuvutia, Ustawi wa Wanyama, Usawa wa Kijamii, Utunzaji Wazee Kujitolea na Uhisani, Kusaidia Jamii za Vijijini na Maeneo ya Mbali, Kutatua Migogoro na Kujenga Amani, Kilimo Endelevu na Uhakika wa Chakula.
Elimu Jumuishi, Afya ya Akili na Ustawi, Ujasiriamali, Mentorship na Uongozi kwa Vijana, Nishati Safi, Msaada kwa Wakimbizi na Wahamiaji, Kuwezesha Wanawake na Wasichana, Maelewano na Umoja wa Kidini, Uhamasishaji wa Elimu, Msaada kwa Watu wenye Ulemavu,Kurejesha Maeneo ya Kihistoria na vivutio vya Kihistoria.

Maeneo mengine ni Kujenga Jamii kupitia Michezo, Upatikanaji wa Teknolojia za Kidijitali, Mradi wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira, Utetezi wa Haki za watu wa Asili na Makabila
Sanaa kwa Mabadiliko ya Kijamii, Dharura na Msaada, Ushiriki wa Kiraia na Uanaharakati wa Jamii, Ubunifu katika Nishati Mbadala, Upatikanaji wa Msaada wa Kisheria na Huduma za Haki, Miradi ya Makazi na Malazi, Miradi ya Mazingira inayoongozwa na Vijana, Kukuza Elimu ya Lugha.
“Pia tutaangalia Msaada kwa Yatima na Watoto katika mazingira magumu, Upatikanaji wa Chakula, Utatuzi wa Migogoro kupitia Sanaa na Muziki, Ulinzi wa Jamii na Usalama kupitia Polisi Jamii, Kukuza Kilimo Endelevu, Shule salama na Jumuishi, Sayansi na Mazingira, Biashara ya Haki, Shujaa wa Huduma za Umma na Ofisa Mzuri wa Kikosi cha Kijeshi/Polisi,” amesema.