Tuchukue tahadhari mvua zinazoendelea kunyesha nchini

MVUA kubwa zinaendelea kunyesha katika mikoa mbalimbali nchini na kusababisha uharibifu katika miundombinu pamoja na kwenye makazi ya watu.
Mikoa ya Tabora, Shinyanga, Mwanza, Morogoro, Kilimanjaro na Dar es Salaam, ni baadhi ambayo imeshuhudia mvua kubwa katika siku za karibuni.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), mvua hizo kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini, zimesababisha athari kubwa katika miundombinu na huduma za usafiri ikiwamo kusababisha hitilafu za umeme zilizoathiri shughuli za Reli ya Kisasa (SGR) mwishoni mwa wiki.
Athari nyingine ni katika miundombinu ya reli ya zamani ya MGR baada ya madaraja kuathiriwa Kidete wilayani Kilosa, Mkoa wa Morogoro, na Gulwe wilayani Dodoma, na katika Barabara Kuu ya Morogoro–Iringa eneo la Mama Marashi hadi Mikumi, ambako maporomoko ya mawe na tope yalisababisha usumbufu wa usafiri wa magari.
Kama hiyo haitoshi, radi imeua mtu mkoani Tabora na kujeruhi wawili kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha ambazo pia zimesababisha athari nyumba kuezuliwa paa, kujaa maji na mafuriko katika maeneo mbalimbali yakiwamo ya Mwanza, Kahama, Kilosa na Tabora.
TMA imetoa tahadhari ya vipindi vya mvua kubwa katika mikoa mingi ikiwamo Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe, Dodoma, Singida, Morogoro, Lindi, Mtwara, Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tanga, Dar es Salaam, Pwani pamoja na Visiwa vya Unguja na Pemba.
Wakati serikali imechukua hatua kadhaa kurejesha hali ya miundombinu katika sehemu mbalimbali, ni muhimu kwa wananchi kuchukua tahadhari wakati huu ambao mvua zinaelezwa kuwa zitaendelea kunyesha.
Katika hili, wananchi wanapaswa kuendelea kufuatilia taarifa za utabiri na kuzingatia ushauri wa wataalamu ili kujikinga na athari zinazoweza kujitokeza.
Kama hiyo haitoshi, jukumu jingine la wananchi ni kuendelea kuweka mazingira yao katika hali ya usafi ikiwamo kuzibua mitaro iliyoziba, kukagua uimara wa nyumba zao hasa paa na kuta ili kuhakikisha mvua zenye upepo mkali haziathiri makazi yao.
Pia, ujengwe utamaduni wa kuvuna maji ya mvua kwani tumeshuhudia maeneo mengi maji haya yakiachwa bila kutumika na kusababisha athari kubwa zikiwamo za mafuriko na nyinginezo.
Kama maji haya yakivunwa, si tu yataondoa maafa kwa wananchi, bali yatatumika kwa shughuli nyingine muhimu katika ustawi wa maisha ya Watanzania.
Kwa mamlaka za serikali hasa zinazoshughulika na miundombinu ikiwamo ya barabara na madaraja, ni muhimu katika kipindi hiki kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa miundombinu hiyo kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza ikiwamo kuvunjika kwa madaraja na barabara na hivyo kuleta usumbufu kwa watumiaji.



