TUCTA yawasilisha hoja 9 muswada sheria ya kazi

Rais wa Tucta, Tumaini Nyamhokya.

SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) limewasilisha kwa Kamati ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii hoja tisa kuhusu marekebisho ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Kazi kwa Mwaka 2024.

Kati ya hoja hizo, imo inayohusu likizo ya dharura isiyo na malipo kwa mfanyakazi iwe angalau miaka mitano badala ya siku 30 zilizopendekezwa kwenye muswada na pendekezo kuwa endapo mama atajifungua mtoto njiti apewe muda wa uangalizi wa mtoto mpaka akamilishe wiki 40 badala ya wiki 36 zilizopendekewa katika marekebisho ya sheria hiyo.

Akizungumza jijini Dodoma baada ya kuwasilisha maoni kwa kamati hiyo, Rais wa Tucta, Tumaini Nyamhokya amesema lengo la kuongezwa kwa muda wa  likizo ya dharura ni kukidhi mahitaji ya mtu anayekuwa kwenye mchakato wa kiuongozi au kimasomo.

Advertisement

“Hii itamsaidia mfanyakazi anyeomba likizo ya dharura ambayo haitakuwa na malipo kwa mfanyakazi mwenye uhitaji kwenda kutumia lengo lake, mfano anagombea uongozi hatua kwenye vyama vya wafanyakazi itampa fursa ya kutumikia na baadaye kurejea kwa mwajiri ili ampangie majukumu mengine,” amesema.

Nyamhokya amesema Tucta pia, imependekeza kuwa mfanyakazi anayeajiriwa kwa misingi ya kupata mafunzo afanye mafunzo hayo kwa kipindi cha miezi isiyozidi 12 kisha aajiriwe kama mfanyakazi kamili badala ya miezi 24 iliyopendekezwa na muswada.

“Muswada unapendekeza kwenye masuala ya dharura/majanga mwajiri akae na mfanyakazi kukubaliana namna ya kushughulikia hilo suala. Maoni ya Tucta ni kuwa pale ambapo kuna chama cha wafanyakazi mwajiri ashauriane na
chama hicho ili kulinda haki na maslahi ya wafanyakazi. Mfano, hatma ya ajira na ujira kwa mfanyakazi,” amesema.

Tucta pia, inashauri nafuu ya mtu anayesitishiwa ajira kwa kutokufuata taratibu au kutokuwapo na sababu zenye mashiko alipwe fidia au nafuu ya mishahara kulingana na sheria iliyopo sasa.