‘Tufuatilie nyumba za starehe kudhibiti maadili’

DAR ES SALAAM: SERIKALI imetakiwa kuchukua hatua madhubuti kwa kuwakagua na kuwafuatilia kwa karibu wamiliki wa nyumba za starehe pamoja na waandaaji wa matamasha mbalimbali ili kuhakikisha wanazingatia maadili. Lengo kuu ni kuzuia kuendelea kwa mmomonyoko wa maadili unaozidi kushamiri nchini.

Wito huu umetolewa leo Aprili 22, 2025 na Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kijitonyama, Eliona Kimaro. katika semina ya maadili iliyowalenga watumishi wa Wizara ya Michezo na Utamaduni pamoja na wakurugenzi wa halmashauri mbalimbali.

Semina hiyo imefanyika katika Ukumbi wa Julius Nyerere, ambapo Mchungaji Kimaro amewaasa viongozi waliopewa dhamana ya kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan kutoa elimu ya malezi bora kwa jamii. Ameeleza kuwa jukumu la malezi si la familia pekee bali ni la jamii nzima, hasa wale waliokabidhiwa dhamana ya uongozi.

Akiendelea na hotuba yake, Mchungaji Kimaro amesema kuwa mmomonyoko wa maadili ni tatizo la kimataifa linalohitaji juhudi za pamoja kulikabili.

Ameahidi kuwa viongozi wa dini wataendelea kuhubiri, kufundisha na kuwa mfano bora kwa jamii ili kuonyesha namna binadamu anavyopaswa kuishi kwa kuzingatia maadili mema.

Ameeleza kuwa kizazi cha maadili hakijengwi kwa siku moja bali ni matokeo ya urithishwaji wa maadili kutoka kizazi kimoja kwenda kingine. Hivyo, juhudi za makusudi zinahitajika katika kuhakikisha vijana wa sasa wanalelewa katika misingi imara ya maadili.

Mchungaji Kimaro ametoa wito kwa vyombo vya habari kuwa vinara wa kusambaza elimu ya malezi kwa jamii kwa kutumia majukwaa yao kufikisha ujumbe chanya. Amesisitiza kuwa vyombo hivyo vina nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko chanya endapo vitatumika ipasavyo katika kampeni ya kurejesha maadili nchini.

Habari Zifananazo

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button