TUGHE kuboresha maslahi ya wanachama wake

MOROGORO: Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) kimesaini Mkataba wa Hali Bora ya Watumishi wake unaolenga kuboresha maslahi yao katika maeneo mbalimbali.

Katika taarifa ya TUGHE iliyotolewa jana Desemba 10, 2023 na kusainiwa na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Hery Mkunda imesema kuwa kwa mara ya kwanza Mkataba umeongeza idadi ya siku kwa mfanyakazi mwanamke atakayejifungua mtoto njiti na kufanya TUGHE kuwa Chama cha kwanza kuweka kipengele hicho katika Mkataba wake wa Hali Bora.

Mkunda amesema kuwa lengo la kuboresha kipengele hicho ni kutambua na kuthamini mchango mkubwa unaofanywa na wanawake ndani ya TUGHE hivyo kwa kufanya hivyo kutaongeza tija na ufanisi ndani ya chama hicho.

Aidha, ameiomba serikali kupitia upya na kuboresha sera na sheria mbalimbali zitakazojumuisha wanawake wanaojifungua watoto njiti kama ambavyo TUGHE wameanza kufanya ili kuwapatia muda wa kuwahudumia watoto pamoja na kuimarisha afya zao.

Kwa upande wake Mgeni Rasmi Makamu Mwnyekiti wa TUGHE Taifa, Dk Jane Madete amesema kuwa amefurahishwa na uamuzi huo wa kufikia makubaliano hayo kati ya uongozi na wafanyakazi kwani utaenda kuongeza ari ya kufanya kazi kwa bidii na kukifanya chama kipige hatua mbele zaidi.

Mkataba huo uliosaniwa ni wa muda wa miaka mitatu na una kipengele cha kufanyika kwa marekebisho muda wowote ambapo pande zote mbili zitaona kuna uhitaji wa kufanya hivyo.

Pia Mkataba huo utawahusu wafanyakazi wote walio katika ajira ya kudumu na zile za mikataba ya muda maalumu.

Habari Zifananazo

Back to top button