TUGHE yamuunga Mkono Rais Samia

WAGENI zaidi ya 800 kutoka Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) wamefanya ziara ya kihistoria katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro Jana.

Ziara hiyo ina lengo la kuwaleta pamoja waajiri na wafanyakazi ili kupata uelewa wa pamoja, kujadili na kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza mahala pa kazi.

Ziara hiyo ilifanyika mara baada ya wajumbe wa TUGHE kumaliza semina iliyofanyika jijini Arusha kuanzia Agosti 26.

Akiongoza ujumbe huo Mwenyekiti wa TUGHE Taifa, Joel Kaminyoge amesema lengo la ziara yao ni kutoa hamasa ya utalii wa ndani na kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika kukuza utalii ambapo ziara hiyo imewapa fursa wanachama wao kujionea vivutio vya kipekee vinavyopatikana hifadhi ya Ngorongoro.

“Leo tumekuja na wanachama zaidi ya 800 kutembelea kreta ya Ngorongoro kujionea moja kati ya vivutio bora vya dunia ambavyo ni sehemu ya urithi wa dunia, tunaamini kwamba ziara yetu italeta tija na hamasa kwa wakuu wa taasisi kuwa na utaratibu wa kuwapeleka watumishi wao kufanya utalii wa ndani katika vivutio mbalimbali nchini,” Alisema Kaminyoge

Akiwapokea wageni hao, Meneja wa Huduma za Utalii na Masoko wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Mariam Kobelo alisema mamlaka hiyo ipo tayari kuendelea kupokea makundi mbalimbali ya wageni na kuwahakikishia kuwa wanapata huduma bora.

Mkurugenzi wa Tanzanite Cooperates Ltd, aliyeratibu ziara hiyo Elina Mwangomo, ameleza kuwa kwa sasa kuna ongezeko kubwa la watalii wa ndani hali inayoongeza hamasa kwa wadau wa utalii kuendelea kuboresha huduma zao huku akieleza kuwa Ngorongoro imekuwa moja kati ya eneo ambalo linapendwa zaidi na wageni na watalii kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.

Jackline Ngoda ambaye ni mmoja kati ya wanachama waliotembelea hifadhi hiyo ameonesha kufurahishwa na ziara hiyo baada ya kujionea wanyama mbalimbali ikiwepo wanyama wakubwa watano wakiwa katika maeneo yao ya asili.

“Kwa ujumla tumeona Wanyama mbalimbali, wakiwemo simba, nyati, tembo, swala, nyumbu, viboko, pundamilia na wengine wengi, tumeweza kuona uzuri wa kipekee wa Kreta ya Ngorongoro na napenda kuwaambia watanzania wenzangu waje kutembelea Ngorongoro na kujionea uzuri wake wa asili,” Alisema Jackline.

Ziara hii ni sehemu ya juhudi za TUGHE kuwaleta pamoja waajiri na wafanyakazi wa taasisi za Serikali kupata nafasi ya kujifunza na kujenga uhusiano mzuri na ushirikiano nje ya mazingira rasmi ya kazi.

Habari Zifananazo

Back to top button