Tuipe nafasi Tume ifanye kazi yake
TUME ya Rais ya kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea wakati na baada ya Oktoba 29, 2025 imetaka umma wa Watanzania uiamini, ikiahidi kutekeleza majukumu yake kwa weledi, uadilifu na uwazi ili kuleta majibu sahihi.
Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande alitoa rai hiyo alipozungumza na vyombo vya habari wiki hii akisisitiza isihukumiwe kabla ya kuanza kazi.
Angalizo la mwenyekiti wa tume limejaa busara, likistahili kuheshimiwa na Watanzania wote wanaotambua na kuthamini uungwana. Huu ni mwito muhimu katika kipindi ambacho taifa linahitaji utulivu, umoja na maridhiano kuliko wakati mwingine wowote.
SOMA: Tume kuchunguza mambo 6 vurugu za Okt.29
Katika hekima ya Kiswahili tunafundishwa kuwa ‘Haraka haraka haina baraka. Methali hii inatukumbusha kuwa mambo muhimu, hasa yanayogusa mustakabali wa nchi, yanahitaji kutazamwa kwa umakini na kufanyiwa kazi bila papara.
Subira ni nguzo ya ustaarabu kwani ni tabia inayotofautisha werevu na jazba. Inamuongoza mtu au jamii yoyote kupata majibu sahihi, ya kina na yasiyopotoshwa na hisia za muda.
Ni muhimu kutambua kwamba tume hii imepewa jukumu nyeti la kuchunguza, kusikiliza, kuchambua na kutoa hitimisho lililosheheni ukweli kuhusu matukio yaliyoibua taharuki katika jamii.
Kwa hiyo, ni jukumu linalohitaji muda, uhuru, na mazingira tulivu ya kiutendaji. Ndiyo maana mwenyekiti Chande amesisitiza kuwa tume hiyo itafanya kazi kwa weledi, uadilifu na uwazi.
Isivyo bahati, katika siku za karibuni kumekuwepo na kelele na jazba kutoka kwa baadhi ya makundi, zikionesha taswira ya kutaka tume ihukumiwe kabla haijaanza au kukamilisha kazi yake.
Huu si msingi mzuri kwa taifa linalojitafuta katika ukweli na maridhiano. Tunapaswa kukumbuka usemi mwingine wa hekima: ‘Subira yavuta heri’ kwamba hauna budi kupewa nafasi.
Tukisubiri kwa utulivu, tutavuna majibu yaliyojaa heri kwa taifa zima. Tamko la tume limedhihirisha usikivu na unyenyekevu wake kwa umma wa Watanzania kwani haikupuuza ‘kelele’ hizo za kuikosoa kabla ya kuhitimisha kazi yake.
Badala yake, busara zimeiongoza kuzungumza kwa utulivu na kuhakikishia umma kwamba kazi yake itakuwa na tija. Tume inapofanya kazi katika mazingira ambayo kila upande umejitayarisha kusikiliza na kukubali ukweli, bila shinikizo wala tashwishwi, ni dhahiri matokeo yake yatakuwa na uhalali wa kijamii.
Ndiyo maana tunawasihi wananchi kuwa watulivu, waache tume itimize wajibu wake na waepuke maoni yanayochochea hisia kabla ya hoja rasmi kuwasilishwa.
Ni vyema kuzingatia kwamba, kitendo cha kukurupuka kutoa hukumu kabla ya mchakato kukamilika kinaweza kuharibu taswira ya kitaasisi, kupotosha mwelekeo wa mjadala na hatimaye kuzuia kufikiwa kwa majibu ya haki.
Taifa lenye hekima hujenga mifumo imara na mifumo hiyo haipewi majibu bali hutafuta majibu. Kwa mantiki hii, kuamini tume ni kulinda ustaarabu na uungwana wetu kama Watanzania.
Kwa hiyo, tunaendelea kutoa rai kwa Watanzania wote bila kujali mitazamo yao, kuwa watulivu, waendelee kuiamini tume na kwa utulivu wasubiri matokeo.
Muda ukifika tume ikatoa ripoti yake, ndipo iwe nafasi ya kuuliza, kuchambua na kutoa hoja kwa misingi ya taarifa sahihi na si hisia.



