Tuipe ushirikiano Tume ya Uchunguzi

RAIS Samia Suluhu Hassan ameteua na kuizindua Tume Huru ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Ameiteua tume hiyo Novemba 18, mwaka huu ikiongozwa na Jaji Mkuu mstaafu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman na jana aliizindua katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma. Tume hiyo ina jumla ya wajumbe wanane. Pamoja na mambo mengine, Rais Samia ameielekeza tume hiyo kuchunguza mambo kadhaa, ikiwamo fedha wanazodaiwa kupewa vijana walioandamana zimetoka wapi.
Maeneo mengine ni kuchunguza madai ya vijana kutaka haki, ni haki gani hiyo waliyoikosa ili serikali iwapatie, kuangalia ushiriki wa taasisi zisizo za serikali (NGO) za ndani na nje ya nchi katika vurugu hizo, sababu hasa ya vijana kuingia barabarani na kufanya vurugu na kujua kiini cha tatizo hilo. Kwa mujibu wa Rais Samia, tume itakapokabidhiwa makabrasha ya kufanyia kazi, itakabidhiwa na hadidu za rejea watakazokwenda kuziangalia na kuzifanyia kazi.

Wakati akizindua Bunge la 13 jijini Dodoma hivi karibuni, Rais Samia aliahidi kuunda Tume ya Uchunguzi wa vurugu za siku ya uchaguzi na baada ya uchaguzi na jana alieleza tume hiyo imeundwa kwa mujibu wa Sheria ya Tume za Uchunguzi ya Mwaka 2023 Sura ya 32 ambayo inampa rais mamlaka ya kuunda tume mbalimbali. SOMA: Tume Uchunguzi vurugu Oktoba 29 yazinduliwa
Tunampongeza Rais Samia kwa uamuzi huo ambao kwa kiasi kikubwa unakwenda kutoa picha ya nini hasa kilichotokea wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29 na baada ya siku hiyo, katika hali hii ambayo haijawahi kulikumba Taifa la Tanzania. Sisi tunaamini tume hiyo itakuja na mawajabu ya sababu hasa za vijana hao kuingia barabarani na kufanya vurugu na uhalifu ulioshuhudiwa siku hiyo na kupendekeza njia za kukabiliana na hali hii siku za baadaye.
Tunasema hivyo kwa sababu wajumbe wa tume hii ni watu wanaoaminika katika jamii ya Tanzania kutokana na uzoefu wao katika masuala mbalimbali ndani na nje ya nchi, hivyo kuwa katika nafasi nzuri ya kutumia weledi wao kulisaidia taifa.

Ni kwa msingi huo, tunawaomba wale wote watakaoitwa mbele ya tume kuisaidia katika kutekeleza majukumu yao kufanya hivyo, kwani mchango wao ndio utakaosaidia kupata suluhisho la kwenda kuliponya taifa hili kutokana kadhia ile, badala ya kuendelea kunyoosheana vidole vya lawama.
Pia, kama alivyoeleza Rais Samia mapendekezo ya Tume ya Uchunguzi ndiyo yatakayofanywa ajenda kwenye Tume ya Maridhiano, hivyo ni muhimu wote wenye mawazo ya kujenga taifa kuipa ushirikiano Tume ya Jaji Othman ili kuhakikisha Tanzania inatoka hapa ikiwa salama na inaendelea kuwa nchi salama ya kuigwa mfano katika amani, umoja na mshikamano wa watu wake.



