Tume ya Ardhi yaja kuongeza usimamizi

SERIKALI imesema inakusudia kuanzisha Tume ya Taifa ya Ardhi.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi amesema pamoja na mambo mengine tume hiyo itaweka mfumo wa usimamizi na utekelezaji wa shughuli za ardhi.

Amesema hayo Dodoma wakati akieleza mafanikio ndani ya miaka minne tangu, Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani.

Alisema serikali imeendelea kuongeza uwekezaji katika sekta ya ardhi ili kuongeza kasi ya kutambua, kupanga, kupima na kumilikisha ardhi kwa matumizi mbalimbali, ikiwemo uwekezaji.

Ndejembi alisema tume hiyo itaweka mfumo wa usimamizi na utekelezaji wa shughuli za sekta ya ardhi katika ngazi zote hivyo kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya sekta hiyo.

“Tunataka mambo yote ya mipango miji, upimaji, utoaji wa vibali vya ujenzi yaratibiwe sehemu moja.”

Akaongeza: “Hii itaondoa changamoto katika sekta ya ardhi, ikiwamo migogoro ya ardhi inayotokana na kukosekana usimamizi madhubuti na kukosa uadilifu kwa watumishi.”

Kwa mujibu wa Ndejembi, wakati umefika kuanzisha chombo kitakachosimamia mawakala wanaofanya biashara au wanaojihusisha na masuala ya ardhi wasajiliwe, watambuliwe na maeneo wanayofanyia kazi.

“Kwa sasa tupo katika hatua za mwisho kuhakikisha kunakuwa na chombo cha kuwasimamia na kuwalinda Watanzania wanaonunua ardhi au waliopo sekta ya miliki ya ardhi,” alisema Ndejembi.

Alisema pia wizara imepanga kuandaa ramani za msingi kwa kutumia Sh bilioni 65 na imepanga kukamilisha kazi hiyo mwaka 2030 kuziboresha ramani zinatumika sasa zilizoandaliwa mwaka 1960 na 1970.

“Wizara imekusudia kupiga picha za anga kwa kutumia ndege yenye rubani na zisizo na rubani, hatua itakayosaidiwa kuandaa ramani za msingi kwa nchi nzima zenye taarifa za kijiografia,” alisema Ndejembi.

Alisema wizara imeandaa programu ya uendelezaji upya maeneo yaliyochakaa katika miji nchini itakayosaidia kuboresha huduma za msingi katika maeneo hayo na hivyo kuyawezesha kuchangia katika Pato la Taifa.

Aidha, alisema serikali imekamilisha Marekebisho ya Sera ya Taifa ya Ardhi ya Mwaka 1995 (Toleo la Mwaka 2023) yanayolenga kuweka mfumo madhubuti wa umiliki wa ardhi, usawa katika upatikanaji ardhi, usimamizi na matumizi ya ardhi kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii na kuendelea na marekebisho ya sheria mbalimbali kuhusu sekta ya ardhi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button