Tume ya Jaji Chande yatua Mara

TUME ya Rais inayochunguza matukio ya uvunjifu wa amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka jana imeanza kazi yake mkoani Mara, ikiwa na lengo la kukusanya maoni na ushahidi kutoka kwa makundi yaliyoathiriwa na matukio hayo. Uchunguzi huo unalenga kubaini ukweli wa matukio ya uchaguzi na kipindi cha baada ya uchaguzi, yaliyosababisha kupoteza maisha kwa baadhi ya wananchi, wengine kujeruhiwa na uharibifu wa mali.

Akizungumza Mjumbe wa tume hiyo, Balozi Radhia Msuya alisema lengo la tume hiyo ni kubaini namna ya kukabiliana na changamoto zilizojitokeza kutokana na matukio hayo hasa ikizingatiwa kuwa hali kama hiyo haijazoeleka nchini hivyo kutafuta njia mwafaka za kuzuia kutokea tena kwa matukio ya aina hiyo. Balozi Msuya aliongeza kuwa ziara ya siku tatu ya tume hiyo katika wilaya za Tarime, Bunda na Musoma itajikita katika kuchunguza kilichotokea, athari zilizojitokeza, pamoja na mapendekezo ya namna ya kusonga mbele kama taifa.

Mjumbe mwingine Balozi David Kapya amesema wamefika Mara kusikiliza uongozi wa mkoa na wadau ili kufafanua hali halisi ilivyokuwa, kupokea ushauri na kuwasilisha mapendekezo yao kwa Rais Samia Suluhu Hassan ili hatua stahiki zichukuliwe.SOMA: Wadau watarajia ripoti ya tume kuimarisha umoja

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi amesema mkoa huo hautaki kurejea katika machafuko yaliyotokea awali na kwamba wananchi wa Mara wana matumaini makubwa na tume hiyo. “Kila mmoja anaitazama tume hii kama chombo cha kutuelekeza na kutuonesha namna ya kutoka katika changamoto hizo, kwani hatupendi na hatutaki kurudia tena hali hiyo,” alisema Mtambi.

Ikiwa mkoani Mwanza juzi, baadhi ya wananchi waliofika mbele ya tume walidai chanzo cha vurugu hizo kilikuwa ni pengo kati ya waliokuwa nacho na wasiokuwa nacho. Walidai pengo hilo linasababishwa hasa na ukosefu wa ajira kwa vijana ikizingatiwa mfumo wa elimu wa miaka iliyopita ulikuwa ukiwaandaa wahitimu kuajiriwa na si kujiajiri. Kiongozi wa waendesha bodaboda Kata ya Luchelele wilayani Nyamagana, Seif Zingiye alisema eneo hilo lina takribani vijana 400 wanaojihusisha na shughuli hiyo ya usafirishaji wakiwamo wahitimu wa vyuo vikuu ambao hajafanikiwa kuajiriwa, licha ya kuwa na fani mbalimbali.

“Wanatuambia wamehudhuria usaili mara kadhaa bila mafanikio. Kibaya zaidi, bado wapo wasaili waliogubikwa na rushwa pamoja na ukabila au undugu. Wanawapatia kazi wale wanaowahitaji wao. Hii inawakatisha tamaa wengine na kuwafanya warubunike kiwepesi kushiriki maandamano ya hatari,” alisema.

Mwenyekiti wa machinga soko la Kisesa wilayani Magu, Daniel Ouko alitolea mfano jinsi ambavyo wamekuwa wakilazimishwa kuhamia soko jipya la Kayenze ambalo halina miundombinu yoyote, hali iliyowasukuma baadhi yao kushiriki maandamano.

Naye Anastazia Wambura alisema alikuwa msimamizi wa uchaguzi kituo cha kupigia kura cha Pamba, aligundua vurugu zilisababishwa na mfumo dume kwani baadhi ya wanaume walikuwa wakihoji kwa nini CCM imemweka mgombea urais mwanamke. Amesema hata alipowauliza kwanini asiwepo mwanamke ikizingatiwa awamu ya utawala uliopita ametekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, hawakuwa na jibu. Kiongozi wa Tume kwa Kanda ya Ziwa, Balozi Ombeni Sefue aliwasihi Watanzania kuendeleza mshikamano, umoja na upendo ili kuirejesha Tanzania katika hali ya amani.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button