Tume ya Mipango yazitaka serikali za mitaa PPP

TUME ya Mipango imesema ni muhimu kushirikisha serikali za mitaa katika utekelezaji wa miradi kwa ubia katika sekta ya umma na sekta binafsi (PPP).

Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango (Masuala ya Kitaifa), Dk Mursali Milanzi amesema serikali za mitaa wana miradi mingi ambayo ingeweza kutekelezwa kwa kupitia PPP lakini haitekelezwi.

Dk Milanzi amesema hayo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwenye kongamano la kuhusu nafasi ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi katika kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

“Maisha yetu yote yapo huko (serikali za mitaa) na huko ndiko ambako kuna vyanzo vingi, kuna mahitaji makubwa na ndipo kutakuwa na chimbuko la maendeleo, sasa serikali za mitaa zikoje?

Kuna changamoto za kukabili, lakini tunapoiangalia Dira ya 2050 tunataka serikali za mitaa ziwe za namna gani? Ziwe na uhuru wa kutosha? Au tunataka ziendeleee kutegemea Serikali Kuu,” alihoji Dk Milanzi.

Dk Milanzi alisema kama serikali za mitaa zitaendelea kujiendesha kwa kutegemea serikali kuu mambo hayatakuwa na tija. “Na kama zitakuwa na uhuru ni uhuru wa namna gani utakaotupatia tija?” alisema.

Dk Milanzi na kuongeza kuwa Dira ya 2050 ingependa kuona serikali za mitaa zinapata nafasi ya kufanya maamuzi bila kutegemea Serikali Kuu.

“Ila kama ni uhuru tuangalie ni aina gani ya uhuru ambayo serikali za mitaa itapata ili kutekeleza, lakini tunapotaka serikali za mitaa ziingie PPP, je tumewaandaa namna gani, lazima tuwaandae kuingia huko, wenzetu wana programu nyingi za kujenga uwezo,” alieleza.

Dk Milanzi alisema kutekeleza yaliyomo kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kama nchi ina nafasi ya kufanya vizuri iwapo kutakuwa na mabadiliko ya namna ya mambo yanavyofanywa sasa vinginevyo nchi haitapiga hatua.

Alisema Dira ya 2050 imetokana na matamanio ya wananchi waliotoa maoni yao kuhusu nchi gani wanaitaka na moja ya mambo yaliyotakiwa ni kutaka kuwa kwenye uchumi wa thamani ya Sh trilioni moja jambo ambalo litalazimu kuwe na kazi ya kufanya ili kufikia malengo hayo.

“Na hapo tunazungumzia pato la mtu mmoja mmoja, inatakiwa isipungue kiasi cha Dola 7,000 hivi (takribani Sh milioni 20) na sasa tupo kwenye Dola 1,280 hivi (takribani Sh milioni tano), sasa miaka 25 ijayo tunaitafuta Dola 7,000 hiyo inatupa picha kwamba huko tunapokwenda tunatakiwa sisi tusiwe watu wa kawaida kwa namna tunavyofikiri na tunavyotekeleza mipango yetu bila hivyo tutarudi palepale,” alisema Dk Milanzi.

Alisema Dira ya 2025 imetekelezwa vizuri na imesaidia kukuza uchumi mpaka nchi ilipofikia. “Kwa wastani takwimu zinatuonesha kwamba tumecheza kwenye asilimia sita ya ukuaji wa uchumi,” alisema.

Dk Milanzi alisema katika ukuaji wa uchumi huo sehemu kubwa imetokana na uwekezaji uliofanywa na serikali na hiyo tafsiri yake ni kwamba mchango wa sekta binafsi kwenye uwekezaji mkubwa ni ndogo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button