Tume ya uchaguzi yaja na majibu rufaa za madiwani

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imepitia, imechambua na kuzifanyia uamuzi rufaa tatu za wagombea Udiwani zilizowasilishwa kwa Tume.
Taarifa iliyotolewa na mkurugenzi wa uchaguzi wa tume hiyo, Dkt Wilson Charles leo Disemba 6, 2022 Dodoma imesema rufaa hizo zimewasilishwa kufuatia baadhi ya wagombea udiwani kutoridhika na maamuzi ya wasimamizi wa uchaguzi kufuatia mapingamizi yaliyoweka katika zoezi la uteuzi uliofanyika Novemba 30, 2022 katika Kata 12 za Tanzania Bara.
Dk Charles amesema katika kikao hicho tume ilipitia, chambua na kufanyia maamuzi jumla ya rufaa tatu za wagombea udiwani na kutoa maamuzi mbalimbali ikiwemo kukubali rufaa ya ndugu Joseph Machiya kupitia ACT-WAZALENDO.
Kwa mujibu taarifa hiyo Machiya amerejeshwa katika orodha ya wagombea udiwani Kata ya Mwamalili, Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.
Mwingine ni Vitali Maembe (ACT-WAZALENDO) ambaye pia rufaa yake imekubali na karejeshwa katika orodha ya wagombea udiwani Kata ya Dunda, halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo.
Orodha hiyo iliendelea na kumtaja ndugu Samwel Mnyellah (NCCR-MAGEUZI) ambaye rufaa yake imekubali na karejeshwa katika orodha ya wagmbea udiwani kata ya Majohe, halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
“Tume imefikia maamuzi hayo kwa kuzingatia Kifungu cha 44 (5) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292 kikisomwa pamoja na kanuni ya 29(1), (2) na 30 (4) za Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Uchaguzi wa Madiwani), 2020 ambavyo vinatoa fursa kwa wagombea Udiwani kukata rufaa wanapokuwa hawajaridhika na uamuzi wa Wasimamizi wa Uchaguzi kutokana na pingamizi zilizowasilishwa na vinaipa Tume mamlaka ya kukubali au kutengua uamuzi wa Msimamizi wa Uchaguzi,” alisema Mkurugenzi wa Uchaguzi.
Uchaguzi huu Mdogo wa udiwani unafanyika katika kata saba ambazo ni Majohe (Dar es Salaam CC) Dar es Salaam, Mndumbwe (Tandahimba DC) Mtwara, Njombe Mjini (Njombe TC) Njombe, Dunda (Bagamoyo DC) Pwani, Mwamalili (Shinyanga MC) Shinyanga, Mnyanjani (Tanga CC) Tanga, na Vibaoni (Handeni DC) Tanga.
Uchaguzi huo utafanyika sambamba na uchaguzi mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Amani, Wilaya ya Mjini, Zanzibar siku ya Jumamosi, 17 Disemba, 2022.
Taarifa ya mkurugenzi iliongeza kuwa upigaji Kura utafanyika katika vituo vilivyotumika wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 “vituo vitafunguliwa saa moja kamili asubuhi na kufungwa saa kumi kamili jioni,” alisema.