‘Tumieni malighafi sahihi kulainisha vyakula’

DAR ES SALAAM: DAR ES SALAAM: Shirika la Viwango Tanzania (TBS), limetoa wito kwa jamii ya Watanzania kutumia malighafi zilizo sahihi katika kulainisha vyakula.

Hayo yamesemwa leo Februari 13, 2024 na Kaimu Meneja wa Kitengo cha Kufanya tathmini vihatarishi vya chakula kutoka TBS, Ashura Katunzi akizungumzia usalama wa chakula.

Amesema, jamii ya Watanzania wanapaswa kutumia malighafi zilizo sahihi katika kulainisha vyakula na sio kutumia dawa, vinywaji vikali ili kulainishia akitolea mfano nyama ya utumbo.

Advertisement

Amesema, baadhi ya watu wanaweka dawa za hospitali kwenye nyama ya utumbo wakati wa kuchemsha, ili uive haraka na kwamba  si salama kiafya, au wengine wanatumia vinywaji vikali kulainisha nyama ya kuchoma.

Ametaja kanuni tano ambazo wananchi wanapaswa kuzifuata ili kuepuka madhara ya kula chakula kisicho salama ambacho huathiri afya ya walaji, ambazo ni kuhakikisha mazingira  masafi katika maeneo yote yawe ya biashara au nyumbani.

Kanuni nyingine ni kutenganisha chakula ambacho kimeshapikwa na ambacho hakijapikwa, kilichoiva na kibichi, akitolea mfano nyama mbichi huwezi kuweka karibu na nyama iliyopikwa.

“Mfano kuna nyama umeshaipika imeiva, pembeni unaweka nyama mbichi, nyama mbichi unaweka kwenye friji na vyakula vingine mfano matunda, umeme unakatika maji maji ya nyama yanaingia kwenye vyakula vingine, mtu anatoa tunda bila kuosha anakula, hii haifai, ”amesema Ashura.

Amesema pia, jamii inapaswa kuzingatia kutumia malighafi iliyo bora, mfano waliopo viwandani kutumia matunda safi na salama kwa ajili ya kutengeneza juisi, mboga mboga kulimwa katika mazingira sahihi na salama na ziandaliwe kwa usahihi na usafi.

“Chakula kisipokuwa salama kinaleta athari kwa sisi ambao ni walaji wa chakula, athari za kiafya, kiuchumi na maendeleo kwa ujumla,”amesisitiza.

Kwa upande wa Kaimu Meneja wa Ukaguzi na Uzingatia wa Sheria kutoka TBS, Moses Mbambe amesema katika kudhibiti ubora wa chakula wanazingatia mambo matatu, uhamasishaji uzingatiaji wa viwango katika usindikaji, utayarishaji na uuzaji wa bidhaa za chakula.

Amesema, wajibu na utekelezaji wa sheria za viwango kwa wazalishaji, waingizaji na wasambazaji wa bidhaa za chakula hii wanaifanya kwa kutoa elimu kwa wadau juu ya viwango, katika uzalishaji wa vyakula na matakwa ya sheria za viwango pamoja na kanuni zake na kwamba wamekuwa wakifanya  ukaguzi katika soko, viwanda na bidhaa zinazoingia nchini.