Tunamtakia utendaji uliotukuka Dk. Mwigulu

UTEUZI wa Mbunge wa Iramba Magharibi, Dk Mwigulu Nchemba kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania ameandika ukurasa mpya katika historia ya nchi, akiwa ni wa 12 tangu uhuru.

Rais Samia Suluhu Hassan anamuapisha Mwigulu leo kushika nafasi hiyo ambayo kabla yake, walikuwepo viongozi walioishika kutumikia taifa, wakitanguliwa na Mwalimu Julius Nyerere aliyekuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Serikali ya Tanganyika huru.

Alifuatiwa na Rashidi Kawawa, Edward Sokoine, Cleopa Msuya, Salim Ahmed Salimu, Joseph Warioba, John Malecela, Frederick Sumaye, Edward Lowassa, Mizengo Pinda na Kassim Majaliwa.

Kuteuliwa na kuthibitishwa kwa Dk Mwigulu katika wadhifa huo ni tukio muhimu kwa taifa, serikali na wananchi wote. Kura 369 kati ya kura 371 zilizompitisha Dk Mwigulu bungeni ni ushahidi wa imani kubwa ya wananchi kupitia wabunge kwa uongozi wake. Ni dhahiri kwamba, uteuzi wake umeungwa mkono kwa kiwango cha juu kisichoacha shaka juu ya imani aliyopewa na Rais Samia pamoja na Bunge.

Tunampongeza kwa dhati Dk Mwigulu kwa heshima hii kubwa na dhamana ya kulitumikia taifa katika nafasi ya juu ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita. Hatuna shaka na Dk Mwigulu, ikizingatiwa kwamba ni kiongozi mwenye uzoefu mpana serikalini na kisiasa kutokana na uzoefu alionao, ikiwemo kushika wizara nyeti; Wizara ya Fedha na Mipango, Mambo ya Ndani ya Nchi na Kazi, Ajira na Vijana. Uzoefu huu unamuweka katika nafasi nzuri ya kuendeleza kasi ya utekelezaji wa dira ya Rais Samia inayojielekeza katika maendeleo ya taifa.

Ni matumaini yetu kwamba atakidhi kiu na imani ya Rais Samia kwa kuhakikisha anasimamia serikali yenye umoja, uwajibikaji na matokeo chanya kwa wananchi. Hiki ni kipindi muhimu cha mageuzi ya kiuchumi, kijamii na kisera ambacho serikali imejikita katika kukuza uchumi shirikishi, kuvutia uwekezaji, kupanua fursa za ajira kwa vijana na kuimarisha huduma za kijamii.

Hivyo, nafasi ya Waziri Mkuu ni muhimu ikihitaji ujasiri, umakini, ushirikiano wa karibu na mawaziri pamoja na uelewa wa mahitaji halisi ya wananchi. Hatuna shaka na Dk Mwigulu juu ya ambacho serikali imejikita katika kukuza uchumi shirikishi, kuvutia uwekezaji, kupanua fursa za ajira kwa vijana na kuimarisha huduma za kijamii. SOMA: Mwigulu: Nakuja na fyekeo

Kwa kuwa Rais Samia na Bunge limedhihirisha imani kwake, vilevile wananchi wanatarajia matokeo chanya ya uongozi wake kwa uongozi uliojaa hekima, kujenga umoja ndani ya serikali na kuhakikisha kila wizara inatekeleza wajibu wake ipasavyo kwa manufaa ya Watanzania wote.

Tunaendelea kumpongeza Dk Mwigulu kwa kuaminiwa, tukimtakia afya njema, busara na ujasiri wa kusimamia majukumu yake kwa maslahi ya taifa. Wito wetu kwake ni kuendelea kuwa kiongozi anayesikiliza wananchi, anayejifunza na anayetoa uamuzi kwa haki. Hiyo ndiyo itakuwa njia bora ya kuenzi imani aliyoionesha Rais Samia, wabunge na wananchi kwa ujumla

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button