Waanzisha ushirikiano wa kitaalamu sekta ya ujenzi

OFISI ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Baraza la Taifa la Ujenzi zimeingia makubaliano kwa ajili ya ushirikiano wa kitaalamu katika sekta ya ujenzi.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Hamza Johari amesema, wameamua kuingia makubaliano hayo kwa sababu taasisi hizo zinashabihiana kwenye suala la ujenzi na hasa katika miradi mikubwa ya kimkakati.
Amesema kwa makubaliano hayo wanatarajia kuimarika zaidi kwa ujuzi na umahiri wao katika mikataba ya ujenzi.
“Tumeshuhudia serikali ya Awamu ya Sita ikiendelea na jitihada zake za kufanya miradi mbalimbali mikubwa mikubwa na ya kimkakati ya ujenzi, kwa hiyo sisi kama wanasheria, wataalamu wa ujenzi tunatakiwa kuhakikisha kwamba tunakuwa na ujuzi na utaalamu stahiki kuhakikisha miradi hii ya ujenzi mikubwa mikubwa inafanyika vizuri na mikataba inaandaliwa vizuri, inatekelezwa vizuri na usimamizi wake unakuwa mzuri,” amesema.
Amesema wataalamu wa ujenzi katika Baraza la Taifa la Ujenzi na wanasheria kwa upande wa ofisi yake, lazima wafanye kazi kama timu ili kuhakikisha mikataba ya ujenzi na taaluma yake inafanyika vizuri.
“Ni jambo ambalo tunaamini tukilifanya tukiwa na hati hii ya makubaliano tutaweza kubadilishana wataalamu na kwa kufanya hivyo wataalamu wetu watafahamu masuala haya yanayohusiana na sekta ya ujenzi kwa kina zaidi,” amesema.
Amesema anataka wabadilishane utaalamu kwa kupata ushauri wa kitaalamu katika masuala yote yanayohusu sekta ya ujenzi.
“Lakini pili nilizungumza kwenye mafunzo yetu kule Arusha kwamba mafunzo tunakwenda kuyapa kipaumbele kikubwa sana, na mafunzo yapo ya aina mbalimbali mojawapo ni kubadilishana kama hivi kwa kushirikiana na taasisi nyingine ambao wao wana ubobezi kwenye eneo fulani, tunabadilishana wataalamu na kwa kufanya hivyo unajikuta wataalamu wako wanapata mafunzo stahiki kwa maana wa pande zote mbili Baraza la Taifa la Ujenzi wanapata mafunzo ya kile tunachofanya na sisi tunapata uzoefu wa kile wanachofanya,”amesema.
Amesema jambo lingine ni kushirikiana katika kufanya uchambuzi wa madai yatokanayo na mikataba ya ujenzi na suala la majadiliano ya mikataba ya ujenzi.
“Kwa sababu mikataba ya ujenzi iko tofauti kidogo na mikataba ya huduma,tukae pamoja tuone ni vitu gani tunapaswa kuvizingatia katika mikataba ya ujenzi ili kuhakikisha mkataba huo unakaa vizuri sababu wakati wa utekelezaji wake unaweza kujikuta unakwama kumbe kwenye majadiliano haukuzingatia vitu muhimu matokeo yake ukazaa mkataba ambao hauna vile vitu vya msingi ambavyo Baraza la Taifa la Ujenzi linavifahamu na linasisitiza vizingatiwe katika mikataba ya ujenzi,” alisema.

“Lakini na usuluhishi wa migogoro pia ya mikataba ya ujenzi na yenyewe ina upekee wake ambao sisi tunaamini ni muhimu sana tukayafahamu na masuala mengine mtambuka yanayozingatia sekta ya ujenzi nchini na mambo mengine katika sekta ya sheria ili tushirikiane vizuri,” amesema.
Akilizungumzia hilo Mtendaji Mkuu wa Baraza la Taifa la Ujenzi, Matiko Mturi alisema makubaliano hayo ni fursa kubwa kwao kujifunza na kuchota ujuzi wa kisheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
“Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndiyo inayosimamia na kuhakikisha mikataba yote ya Tanzania iko vizuri na mojawpao ni mikataba ya sekta ya ujenzi kama mnavyojua sasa hivi kuna mikataba mingi ya miradi mikubwa kwa hiyo lilipokuja wzo la kushirikiana tuliona linaoana kabisa na azma yetu ya kuhakikisha miradi ya sekta ya ujenzi inatekelezwa vizuri,” alisema.
Alisema kwa muda mrefu tangu baraza hilo kuanzishwa mwaka 1981 wamefanya mambo ya ujenzi kwa muda mrefu hivyo wanajua vipengele vingi ambavyo huwa vinachangamoto hivyo lilipokuja suala la kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu waliona ni nafasi nzuri kwao.



