Tuzo za muziki kitaifa kufanyika Desemba

TUZO za Tanzania Music Awards (TMA) zimetangazwa rasmi kufanyika Desemba 13, 2025, huku dirisha la maombi kwa wasanii wanaotaka kushiriki likifunguliwa leo Ijumaa na litafungwa Novemba 14, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Dk. Kedmond Mapana, amesema jumla ya vipengele 37 vitashindaniwa katika tuzo hizo, ambavyo vitahusisha nyimbo zilizotoka kuanzia Januari hadi Desemba 2024. “Msanii hataruhusiwa kushiriki na wimbo uliotoka mwaka uliopita au mwaka 2025,” amefafanua Dk. Mapana.

Kwa mujibu wa Dk. Mapana, vipengele vya muziki wa Bongo Fleva vitahusisha tuzo nne ambazo ni Wimbo Bora wa Mwaka, Msanii Bora wa Kike, Msanii Bora wa Kiume, na Mtayarishaji Bora. Aidha, muziki wa Singeli utakuwa na vipengele vya Wimbo Bora wa Singeli, DJ Bora wa Singeli, na Msanii Bora wa Wimbo wa Singeli.

Kwa upande wa muziki wa Hip Hop, kutakuwa na tuzo za Mtayarishaji Bora wa Wimbo wa Hip Hop, Mwimbaji Bora wa Hip Hop, na Wimbo Bora wa Hip Hop.

 

Dk. Mapana amesema wasanii wote wanaotaka kushiriki wanapaswa kuwa wamejiandikisha BASATA na watawasilisha maombi yao kupitia tovuti ya award.basata.go.tz kwa kuchagua kipengele wanachotaka kuwania. “Katika upande wa muziki wa dansi, kutakuwa na vipengele vya Wimbo Bora wa Dansi, Mtayarishaji Bora wa Wimbo wa Dansi, na Msanii Bora wa Muziki wa Dansi,” amesema.

Vilevile, muziki wa Taarabu utakuwa na tuzo za Mwimbaji Bora wa Taarabu, Mtayarishaji Bora, na Wimbo Bora wa Mwaka.

Kwa mujibu wa Dk. Mapana, kutakuwa pia na tuzo za jumla zikiwemo Mwanamuziki Bora wa Mwaka, Albamu Bora ya Mwaka, Mtayarishaji Bora wa Mwaka, Wimbo wa Ushirikiano wa Mwaka, Msanii Chipukizi Bora wa Mwaka, DJ Bora wa Mwaka, Mtumbuizaji Bora wa Mwaka, Mtumbuizaji Bora wa Kike, na Mtumbuizaji Bora wa Kiume.

“Baada ya mchakato wa uteuzi, tutatangaza kamati rasmi pamoja na wadhamini wa tuzo hizo. Kwa sasa, maandalizi yanaendelea chini ya usimamizi wa Baraza la Sanaa la Taifa kwa kushirikiana na Seven Mosha,” ameongeza Dk. Mapana.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button