Ubalozi wa Tanzania nchini Sweden waadhimisha siku ya Kiswahili

UBALOZI wa Tanzania nchini Sweden ukishirikiana na jumuiya za Watanzania waishio nchini humo, umeandaa na kufanikisha maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani jijini Stockholm.
Maadhimisho hayo hufanyika duniani Julai 7 kila mwaka na yalianza mwaka 2022 kutekeleza azimio lililopitishwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mobhare Matinyi alisema serikali imeazimia kukieneza na kukienzi Kiswahili duniani kote.
Kiswahili ni lugha ya kikazi Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa waziri wa zamani wa Usawa na Jinsia nchini Sweden, Nyamko Sabuni, mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Nyamko akitoa hotuba kwa Kiswahili, alieleza Kiswahili kinavyoziunganisha nchi akisema hata anapokuwa Kenya kibiashara huitumia lugha hiyo.
Sherehe hizo zilifana kwa wingi wa vyakula na vitu vinavyoitangaza Tanzania na utamaduni wa Mswahili vikiwemo viungo, maonesho ya mitindo ya mavazi, sanaa za mapambo, ngoma, nyimbo, mashairi na hadithi za watoto.
Shughuli hiyo ilikutanisha zaidi ya watu 500 ambao mbali ya Watanzania wengine, walikuwa ni raia au wenye asili za nchi za Afrika Mashariki na Kati, Waswidi marafiki wa Tanzania na mabalozi na wawakilishi wa nchi za Botswana, China, Eritrea, India, Japan, Kenya, Misri, Nigeria, Rwanda na Zimbabwe.



