DAR ES SALAAM: VIONGOZI wa vyama vya NRA na CCK wamesema uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji uliofanyika wiki iliyopita ulikuwa huru na wa haki.
Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Chama cha NRA, Hassan Kisabya amesema kuwa uongozi wa chama hicho umekaa, kujadili na kuona kwamba uchaguzi wa serikali za mitaa ulikua huru haki, huku akisisitiza kuwa, wameyapokea matokeo ya uchaguzi huo kwa moyo mmoja
Kisabya ameeleza kutokuwa na imani na baadhi ya watu wanaotoa taarifa za kutekwa na kupotea akidai kuwa imekuwa kama mchezo wa kuigiza kila mtu kudai ametekwa ama kupotea.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Kijamii (CCK), David Mwajojele akiwa jijini humo, amesema uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji ulifanyika vizuri huku kukiwa na changamoto ndogo ndogo, akitolea mfano dosari iliyojitokeza kwenye moja ya mkutano wa chama hicho, uliovamiwa na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).