Uchaguzi Mitaa wampa tuzo Asas

Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa kimemtunuku tuzo maalum ya shukrani Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (MNEC), Salim Asas, kwa mchango wake mkubwa katika kujenga chama na kufanikisha ushindi wa kihistoria wa asilimia 99.99 kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024.
Tuzo hiyo ilikabidhiwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daus Yasin, wakati wa mkutano wa Halmashauri Kuu ya Mkoa iliyofanyika leo, mjini Iringa.
Yasin alisema kuwa Asas amekuwa nguzo muhimu katika kuhakikisha CCM inapata ushindi mkubwa kupitia juhudi mbalimbali, ikiwemo kufadhili vikao vya mikakati ya ushindi na kutoa kiasi cha Sh Milioni 12 kwa kila wilaya mkoani humo kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi.
“MNEC Salim Asas ameonyesha mfano wa uzalendo wa hali ya juu na kujitoa kwa dhati kwa maendeleo ya chama. Mchango wake umeleta matokeo mazuri ambayo kila mwanachama anapaswa kujivunia,” alisema Yasin.
Baada ya kupokea tuzo hiyo, Asas alieleza kuwa msaada wake kwa chama ni wajibu wake kama mwanachama mwaminifu wa CCM.

Aliongeza kuwa anafikiria kufungua maktaba maalum ya kutunza tuzo na vyeti mbalimbali anavyopokea kutokana na mchango wake wa kijamii na kisiasa.
Wakati huohuo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa amewataka viongozi wa chama kuanza mapema maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ili kuhakikisha chama kinapata ushindi wa kishindo sawa na ule wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
“Hatuwezi kufanikisha ushindi bila maandalizi thabiti. Pamoja na maelekezo haya natoa onyo kali kwa wanachama walioanza kampeni mapema kinyume na utaratibu wa chama. Naziagiza kamati za siasa za wilaya zihakikishe wanachama hawa wanachukuliwa hatua za kinidhamu,” alisisitiza Yasin.

Aidha, kupitia mkutano huo, wenyeviti wa CCM kutoka wilaya za Iringa Mjini, Iringa Vijijini, Kilolo, na Mufindi walitoa ahadi ya kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha CCM inapata ushindi wa viti vyote vya udiwani na ubunge kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Mkutano huo wa mwisho wa mwaka wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Iringa pia ulijadili masuala muhimu, ikiwemo tathmini ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, hali ya siasa katika mkoa huo, na maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.



