Uchunguzi maabara waimarisha usalama, ubora

KATIKA juhudi za kulinda afya ya jamii, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imejidhatiti
kuhakikisha kuwa dawa na vifaa tiba vinavyotumika nchini ni salama, bora na vyenye ufanisi.
Kupitia uwekezaji mkubwa katika miundombinu, rasilimali watu na teknolojia, TMDA imejenga
mfumo imara wa uchunguzi wa kimaabara unaoleta mageuzi katika sekta ya afya.
Maabara Zilivyobadilisha Mwelekeo
Kwa mujibu wa Dk Danstan Shewiyo, Mkurugenzi wa Huduma za Maabara, TMDA ina jumla
ya maabara tatu kuu: Dar es Salaam, Mwanza, na Dodoma. Maabara hizi hufanya uchunguzi wa
dawa, vifaa tiba, malighafi na vitendanishi kabla ya kuruhusiwa sokoni.
Mbali na hizo, anasema kuna maabara ndogo 27 (Minilab kits) zilizosambaa katika hospitali za rufaa na
vituo vya forodha, zikiwa mstari wa mbele katika ufuatiliaji wa bidhaa zinazodhibitiwa.
”Maabara hizo zimepewa ithibati ya kimataifa kupitia Shirika la Afya Duniani (WHO), ikiwa ni hatua
muhimu inayodhihirisha viwango vya kimataifa vya kazi za TMDA.”
Uwekezaji Wenye Matokeo
“Kutoka sampuli 800 kwa mwaka 2021 hadi kufikia 5,700 mwaka 2025 – huu ni ushahidi kuwa
uwezo wetu wa kuchunguza umeimarika kwa kiwango kikubwa’”anasema Dk Shewiyo kwa
fahari. Anaongeza kuwa idadi ya wataalamu imeongezeka kutoka 28 hadi 42 katika kipindi
hicho, ikimaanisha ongezeko la ufanisi na kasi ya utekelezaji wa kazi.
Aidha, mafanikio ya kuongezeka kwa maabara na wataalamu yameleta ongezeko la utoaji
huduma kwa wananchi, huku TMDA ikijipanga kuendelea kusogeza huduma hizi karibu zaidi na
wananchi wote nchini.
Sampuli Zina Sauti
Anasema Katika kuhakikisha bidhaa zilizo sokoni ni salama, TMDA hufanya ukaguzi wa soko (Post-
Marketing Surveillance), usajili wa bidhaa na uchunguzi wa bidhaa kutoka nje ya nchi. Vituo vya
forodha pia ni maeneo muhimu ambapo maabara ndogo hutumika kuchunguza bidhaa kabla
hazijaingia sokoni.
“Kiwango cha ufaulu wa sampuli kimepanda kwa kasi kutoka asilimia 91 mwaka 2021 hadi
asilimia 99.7 mwaka 2024 jambo linaloonesha kuimarika kwa ubora wa bidhaa zinazowasili
nchini. Kwa wale tunaoshirikiana nao kimataifa, tunabadilishana uzoefu bila malipo. Lakini kwa nchi
ambazo hatuna makubaliano, gharama ni dola 800 kwa kila sampuli,” anafafanua Dk Shewiyo.
Maabara ni Jicho la Serikali
Dk Shewiyo anasisitiza kuwa maabara si tu sehemu ya kuchunguza, bali ni kiungo muhimu kati
ya serikali, jamii na sekta binafsi. Kupitia tafiti na mafunzo yanayotolewa na TMDA, wadau
wengi wa afya wameweza kuongeza maarifa juu ya matumizi salama ya dawa na vifaa tiba.

Forodha na Kanda ya Magharibi: Kazi Inaonekana
Katika Kanda ya Magharibi, Meneja wa Kanda, Christopher Migoha, anasema sampuli
zimeongezeka kutoka 65 mwaka 2021 hadi 247 mwaka 2025. Pia, dawa duni zimepungua sokoni
huku vibali vya dawa zenye asili ya kulevya vikitolewa kwa umakini zaidi.
“Jamii bado inahitaji taarifa sahihi kuhusu dawa na vifaa tiba. Hili ni jukumu la pamoja, na
vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika hilo”anasema Migoha.
Viwanda vya Ndani: Ndoto Inayoanza Kutimia
Kwa mujibu wa Dk Yonah Mwalwisi, Mkurugenzi wa Dawa za Binadamu na Mifugo, Tanzania
inaagiza zaidi ya asilimia 80 ya bidhaa tiba kutoka nje. Hata hivyo, idadi ya viwanda
imeongezeka kutoka 13 mwaka 2020 hadi 18 mwaka 2025 – hatua inayoonesha dira ya
kujitegemea. Viwanda sita kati ya hivyo vinazalisha dawa za mifugo, ingawa kwa kiwango
kidogo.
Sauti ya Mtumiaji Inasikika
TMDA imeanzisha mfumo wa kuripoti madhara ya dawa kupitia simu za mkononi kwa kutumia
*152*00# au mfumo wa kielektroniki (ADR Reporting Tool).
Mkurugenzi wa Vifaa Tiba na Vitendanishi, Dk Kisa Mwamwitwa,amesema mfumo huu umesaidia kuongezeka kwa taarifakutoka 5,132 mwaka 2021 hadi 15,623 mwaka 2025.
“Kwa sasa, tuna mifumo madhubuti ya ufuatiliaji. Mtumiaji si tu mteja bali ni sehemu ya mfumowa ulinzi” anasema Dk Mwamwitwa huku akisisitiza usalama wa watoa taarifa.
Nguvu ya Elimu ya Jamii
TMDA inaendelea kushirikiana na vyombo vya habari kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya
dawa na vifaa tiba. Uhusiano huu umesaidia kuongeza uelewa wa jamii na kushusha uwepo wa
bidhaa hafifu sokoni.
“Waandishi wa habari ni sauti ya wananchi. Tunawategemea kuhamasisha
umma utoe taarifa juu ya bidhaa duni na zisizosajiliwa,” anasema Dk Mwamwitwa.



