UDSM kujadili nafasi ya vijana Afrika

DAR ES SALAAM: Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kupitia Ndaki ya Sayansi za Jamii, kimeandaa Mkutano wa Kimataifa wa Sauti ya Sayansi za Jamii (VSS2026), utakaowakutanisha wanataaluma, watafiti na vijana kujadili nafasi ya kizazi cha Gen Z katika kuamua mustakabali wa jamii za Afrika.

Mkutano huo unatarajiwa kufanyika Novemba 5 na 6, 2026, katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ukiwa na kaulimbiu isemayo “Kutafakari Upya Leo na Kesho: Kizazi cha Gen Z na Harakati za Kijamii Barani Afrika.”

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mhadhiri Mwandamizi na Mkuu wa Ndaki ya Sayansi za Jamii ya UDSM, Dk. Richard Sambaiga, amesema mkutano huo unalenga kutoa jukwaa la kujadili mchango, nafasi na changamoto zinazowakabili vijana wa kizazi hicho katika maendeleo ya jamii.

Amesema mijadala hiyo itajikita katika nafasi ya vijana kwenye uongozi, utawala, uwajibikaji wa taasisi za umma na ushiriki wao katika mijadala ya kitaifa, pamoja na namna wanavyoweza kuchangia kujenga jamii yenye uwazi na ushirikishwaji.

Aidha, amesema mkutano huo utajadili mchango wa teknolojia za kidijitali na mitandao ya kijamii katika kuibua mijadala, kusambaza taarifa, kuhamasisha mabadiliko ya kijamii na kuwawezesha vijana kushiriki katika kutafuta suluhisho la changamoto zinazoikabili jamii.

Masuala mengine yatakayojadiliwa ni pamoja na changamoto za ajira, fursa za kiuchumi, mazingira ya kujipatia kipato, jinsia, mahusiano ya kijamii, utambulisho, tofauti za kipato, mabadiliko ya tabianchi, utamaduni, elimu na uzalishaji wa maarifa.

Dk. Sambaiga amesema mkutano huo utashirikisha wanataaluma, watafiti, vijana, wawakilishi wa asasi za kiraia na wadau mbalimbali kutoka Tanzania, nchi nyingine za Afrika na nje ya bara hilo kwa lengo la kubadilishana uzoefu na mawazo kuhusu nafasi ya kizazi cha Gen Z katika kuunda mustakabali wa jamii za Afrika.

Amesema kupitia mkutano huo, wanatarajia sauti, mawazo, matarajio na mahitaji ya vijana kupata nafasi katika mijadala na maamuzi yanayohusu maendeleo ya jamii na mustakabali wa bara la Afrika.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button