UDSM waja na mtaala kilimo biashara
CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kupitia Shule Kuu ya Biashara waanzisha programu ya kufundisha mtaala wa kilimo ili kusaidia vijana kujiajiri na kuajiri wengine.
Akizungumza leo wakati wa uzinduzi wa programu hiyo, Kaimu Mkuu wa Shule ya Biashara wa chuo hicho, Dk Latifa Mbelwa amesema kuwa wanataka shule kuu ya biashara iendane na soko na mahitaji ya nchi kwenye sekta ya kilimo.
“Sekta ya kilimo ina mchango mkubwa kwenye mapato ya nchi inaajiri vijana wengi kwa kiasi kikubwa na jamii ya watanzania, ni sekta inayowabeba wengi,”amesema Dk Mbelwa.
“Tupo kwenye kupitia programu zetu ni kipindi cha kuingiza ujuzi muhimu kwenye mitaala hii baada ya miaka kadhaa tutaweza kutoa wataalamu wazuri wa biashara kwenye maeneo ya uhasibu wa masoko, benki kwenye ujuzi wa kilimo biashara.” Ameongeza Dk Mbelwa.
Amesema “Serikali inafanya makubwa kwenye kilimo kwa sasa hivi kuna mradi makubwa vijana wanaufanya na sisi tunalenga vijana wa vyuo vikuu waondoke na elimu hiyo na ujuzi itakayoleta tija kwenye sekta ya kilimo itakayosaidia uchumi wa nchi kubadilisha kuondokana na umaskini na kutuvusha kwenye ukuwaji wa uchumi wa juu zaidi.”
Mkurugenzi wa Umoja wa Wahitimu Wajasiliamali Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUGECO) Revocutus Kimario amesema wamejikita kufanya kazi na vijana waweze kujiajiri kupitia sekta ya kilimo kwa kubadiri fikra na mitazamo yao wakiona kilimo waone ni fursa ya biashara.
“Kuna programu tunashirikiana na UDSM kufundisha ujasiriamali kwenye sekta ya kilimo inayolenga kuwaongezea vijana ujuzi na maarifa ya kutenda na kuwekeza kwenye kilimo kama fursa itakayowasaidia wao kujiajiri na kutengeneza fursa za kuajiri wengine.” Amesema Revocutus Kimario