Ufaulu mitihani NBAA wapanda

DAR ES SALAAM, Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) imeidhinisha matokeo ya mitihani 100 ya bodi hiyo iliyofanyika Novemba 2024, yakionesha ongezeko la ufaulu kutoka asilimia 66.4 mwaka jana hadi asilimia 70.3 mwaka huu. Wanaume wameongoza kwa ufaulu katika mitihani hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Pius Maneno, jumla ya watahiniwa 6,908 walifanya mitihani hiyo, sawa na asilimia 91.3 ya waliojiandikisha. Kati yao, wanaume walikuwa 3,802, huku wanawake wakiwa 3,764. Watahiniwa 658, sawa na asilimia 8.7, hawakufanya mitihani kwa sababu mbalimbali.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa kati ya watahiniwa waliokamilisha mitihani yao, 4,858 sawa na asilimia 70.3 walifaulu, huku 1,282 kati yao wakifaulu masomo yote katika ngazi husika, na hivyo kustahili kupatiwa barua za ufaulu. Watahiniwa 3,576 sawa na asilimia 51.7 walifaulu baadhi ya masomo, huku asilimia 29.7 ya watahiniwa wakishindwa mitihani yao.

Advertisement

CPA Maneno ameipongeza idadi kubwa ya watahiniwa waliofaulu na kuwataka wale waliopata changamoto kuto kata tamaa. Amesisitiza juu ya  umuhimu wa kuendelea kujifunza kwa bidii na kutumia vitabu vya kiada na ziada vilivyotayarishwa na bodi hiyo ili kuimarisha ufaulu wao katika mitihani ijayo.

“Tunaamini wale ambao hawajafaulu wataongeza juhudi na kujipanga vyema kwa mitihani ijayo. Bodi itaendelea kuwaunga mkono kwa kuwapatia nyenzo bora za masomo,”  amessema CPA Maneno.

Mitihani ya NBAA ni mojawapo ya hatua muhimu katika taaluma ya uhasibu na ukaguzi wa hesabu nchini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uwajibikaji na weledi katika sekta ya fedha.