Ugoni watajwa kugeuka dili Bukombe

BAADHI ya wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita wamedaiwa kutumia tuhuma ama makosa ya ‘ugoni’ kama chanzo cha kujipatia kipato kwa wanandoa kutoka kwa watuhumiwa.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Katente wilayani humo, Issa Shaaban amesema hayo wakati akizungumza na HabariLeo ofisini kwake alipotembelewa na Kampeni ya Msaada wa Kisheria wa Mama Samia (MSLAC).

Issa amesema baadhi ya wanandoa ama watu wanaoishi kama mke na mme wamekuwa wakitengeneza mazingira ya kukamata ugoni ili walipwe pesa kutoka kwa wachimbaji jambo ambalo linaongeza migogoro ya kijamii.

“Ugoni imekuwa sasa ni kama biashara wanaifanya, au wanaita dili, kati ya mme na mke wanafanya makubaliano, kwa kukutwa ugoni ili walipwe. Sasa jambo hili la ugoni tumekuwa tukilishughulikia zaidi kijamii.

“Mara nyingi kwenye ugoni wanataka mtu alipwe kuanzia shilingi milioni moja, au milioni moja na laki tano inategemea na yule wanayeenda kumfumania ana kipato kiasi gani”, amesema Issa.

Mtoa huduma za msaada wa kisheria (ParaLegal), Stephano Kazyoba amesema kukamata ugoni ni lazima kuwe na ushahidi wa moja kwa moja kwa wahusika kukutwa wakiwa faragha wakishiriki tendo la ndoa.

Amesema mtu yeyote hapaswi kutoa tuhuma za ugoni kwa kuhisi au kwa kusikia badala yake ni kwa ushahidi ama ushuhuda unaojitosheleza ambapo taarifa zitatolewa kwa mashahidi wengine na kisha mabalaza ya usuluhishi.

“Mazingira ya ugoni kwanza yawe ya kuona, lakini pia tusikutupuke hata kwenye mazingira ya kuyashuhudia, lakini tutoe taarifa kwenye ofisi ya mtaa, kijiji na tushirikishe majirani kwa ajili ya ushahidi.

“Walishatoka nje ya nyumba ya kulala wageni, wote wawili yale siyo mazingira ya ugoni ingawa wanatoka gesti lakini utakuwa umechelewa, kwa hiyo kuna mazingira kama hayo yanaweza kukufelisha”, amesema.

Wakili wa kujitegemea kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Esther Safari amesema kwa wanandoa ambao wanaingia kwenye mgogoro wa ugoni ama mgogoro mwingine zipo hatua za kuzingatia.

“Hii ni lazima wa la siyo hiari yule anayetafuta suluhu, pale ataitwa yule mwenzie, kuna hatua ambazo watafuata za usikilizaji, lakini kuna wale ambao hawaelewani wanapewa fomu ya kwenda mahakama ya mwanzo.

“Shauri likifika mahakama ya mwanzo litasikilizwa, kama kuna sababu ya msingi ya kusuluhisha ndoa, kwa sababu siyo sababu zote zinaweza kusababisha ndoa kuvunjika, kwa hiyo wanawapa tu muda wa kuelewana”, amesema

“Ikifikia hatua sasa hamuwezi kuafikiana basi mahakama itatoa talaka, tunasisitiza kwamba hakuna mtu yeyote anaweza kutoa talaka isipokuwa mahakamani tu”, amesema.

Habari Zifananazo

3 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button