Uhusiano bora na walipakodi unavyoongeza mapato TRA

KATIKA siku za karibuni kumekuwa na mapinduzi makubwa ya kiutendaji na ukusanyaji wa kodi ndani ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Hali hiyo inaongeza kiwango cha makusanyo siku hadi siku. Hili linadhihirishwa na makusanyo ya Robo ya Kwanza ya Mwaka wa Fedha 2025/2026.
Ndani ya kipindi cha miezi mitatu, TRA imeendelea kuandika historia mpya ya makusanyo ya kodi kwa kukusanya Sh trilioni 8.97 sawa na ufanisi wa asilimia 106.3 ya lengo la kukusanya Sh trilioni 8.44 katika kipindi cha Robo ya Kwanza ya Mwaka wa Fedha 2025/2026 yaani Julai hadi Septemba, 2025.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, makusanyo hayo ni sawa na ukuaji wa asilimia 15.1 ikilinganishwa na Sh trilioni 7.79 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha uliopita.
Anasema makusanyo yaliyopatikana katika Robo ya Kwanza ya Mwaka wa Fedha 2025/26 ni sawa na ukuaji wa asilimia 104 ukilinganisha na Sh trilioni 4.40 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho wakati Serikali ya Awamu ya Sita ilipoingia madarakani mwaka 2021.
Kwa mujibu wa Mwenda, wastani wa makusanyo kwa mwezi umeongezeka kutoka Sh trilioni 1.47 kwa mwezi mwaka 2021/2022 hadi Sh trilioni 2.99 kwa mwezi kwa mwaka 2025/2026. “Kipekee, kwa mara ya kwanza TRA imekusanya Shilingi trilioni 3.47 kwa mwezi mmoja (Septemba). Hiki ni kiasi kikubwa kuliko miezi mingine ya nyuma kama hiyo,” inasema taarifa ya Mwenda.
Ufanisi huo wa TRA katika kukusanya kodi unawaibua wachumi nguli akiwemo Profesa Abel Kinyondo anayesema
kiwango cha makusanyo ya kodi kinachofanywa na TRA kwa sasa kinaiwezesha nchi kutekeleza miradi yake mingi ya maendeleo kwa fedha za ndani.
Anasema katika siku za karibuni kumekuwa na ongezeko la ulipaji wa kodi kwa hiari kwa wananchi, hali ambayo imeongeza makusanyo ya kodi kwa upande wa TRA.
Kwa mujibu wa Profesa Kinyondo, katika nchi nyingi zilizoendelea ukusanywaji wa kodi umekuwa ukifanyika kwa hiari kutokana na wananchi kupatiwa elimu ya kutosha na kuona kulipa kodi kunawahusu moja kwa moja, hali inayowafanya walipe kodi hata kama ni viwango vikubwa.
“Katika nchi zilizoendelea, kodi inatozwa mpaka asilimia 60 lakini watu wanalipa bila kusukumwa na hii ni kutokana na utamaduni waliojengewa wa kutakiwa kulipa kodi kwa maendeleo ya nchi zao, hivyo na huku kwetu tukiweka misingi hiyo tutapata walipakodi wengi zaidi,” anasema Profesa Kinyondo.
Profesa Kinyondo anasema TRA imekuwa ikifanya kazi kubwa kukusanya kodi na kuziwasilisha kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali zinakopangiwa matumizi. Anasema TRA haihusiki kupanga matumizi hayo, hivyo wanaofanya uamuzi wa matumizi wanapaswa kuzingatia mambo yanayowagusa wananchi ili waone faida ya kulipa kodi.
“Matokeo ya kodi ni miongoni mwa chachu ya kuwafanya wananchi waendelee kulipa kodi kwa hiari maana wataona kuwa kodi inawahusu moja kwa moja kwa mustakabali wa maendeleo yao,” anaeleza.
Anasema elimu zaidi ya kodi itaendelea kutolewa na matunda ya kodi kuonekana wananchi wataendelea kulipa kodi kwa hiari kwa maendeleo ya taifa.
Naye Mtaalamu wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Bakar Mohamed anaipongeza TRA kwa kusimamia kwa vitendo maagizo wanayopatiwa na Rais Samia Suluhu Hassan ya kukusanya kodi bila kutumia nguvu yanayoongeza kiwango cha makusanyo ya kodi.
Dk Bakari anasema ukaribu uliopo baina ya TRA na walipakodi umekuwa chachu ya kuchochea ulipaji kodi kwa wananchi maana tendo la kulipa kodi ni la hiari na pale inapotumika nguvu ni rahisi watu kukwepa. “Ulipaji kodi ni tendo la hiari, hivyo kinachofanywa na TRA ni kuwa karibu na walipakodi,” anasema.
Dk Mohamed anaongeza: “Ni jambo la msingi maana linafanya wajione ni sehemu ya TRA na kuwa kulipa kodi ni miongoni mwa majukumu yao, hivyo ukaribu na walipakodi uendelee kuimarishwa ili kupata kodi zaidi.” Anasema maono ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere yalilenga kuona Tanzania inaondokana na utegemezi.
Kwamba, kinachoendelea sasa ni kuondokana na utegemezi kwa kila mmoja kutimiza wajibu wa kulipa kodi itakayotekeleza miradi inayogusa wananchi moja kwa moja ikiwemo ya afya, elimu, maji na miundombinu. Mtaalam wa Uchumi, George Thobias anashauri TRA kuendelea kutoa elimu ya kodi ili kuongeza wigo wa kodi na idadi ya walipakodi itakayopunguza viwango vya kodi katika siku za usoni.
Anasema kupitia makusanyo makubwa ya kodi kwa TRA, miradi mingi ya maendeleo itatekelezwa na kuleta chachu ya ulipaji kodi kwa wananchi wa mijini na vijijini. Kuhusu makusanyo ya TRA kwa Kipindi cha Robo ya Kwanza ya Mwaka wa Fedha 2025/26,
Mwenda anasema yamechagizwa na mambo kadhaa ikiwemo kuendelea kuboresha uhusiano na walipakodi nchini. Anasema huu ni mwendelezo wa utekelezaji kwa vitendo wa maelekezo ya Rais Samia ya kuendelea kuhamasisha ulipaji kodi wa hiari nchini bila uonevu.
Aidha, TRA imeendelea kuboresha uhusiano na ushirikiano na wizara, taasisi mbalimbali za serikali na mashirika ya kimataifa kuhakikisha wote wanashiriki uhamasishaji wa ulipaji kodi kwa hiari nchini. Kwamba kumekuwa na ongezeko la uwajibikaji wa kulipa kodi kwa hiari miongoni mwa walipakodi.
Anaeleza TRA itaendelea kuweka kipaumbele katika utoaji wa huduma bora zinazozingatia mahitaji ya alipakodi kwa kuwahudumia walipakodi siku za mapumziko (Jumamosi na Jumapili) kupitia ofisi zote za TRA nchini.
Kamishina Mkuu huyo wa TRA anasema hatua hiyo itawezesha biashara kuendelea kufanyika kupitia majadiliano na wafanyabiashara ili kuwawezesha walipe madeni yao ya kodi pasipo kuathiri mwenendo wa biashara
zao.
Katika hatua nyingine, taarifa hiyo inasema ufanisi wa makusanyo uliofikiwa na TRA kwa miezi ya Julai hadi Septemba mwaka huu ni kiashiria chanya kuhakikisha lengo la makusanyo ghafi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 la Sh trilioni 36.066 linafikiwa.
Anasema ili kufanikisha hilo, Menejimenti ya TRA inaendelea kutekeleza kikamilifu maagizo yote ya Rais Samia kuhusu usimamizi wa kodi nchini na uhamasishaji wa ulipaji kodi kwa hiari na kuendelea kuwezesha biashara nchini kupitia ‘Dawati la Uwezeshaji Biashara’.
Anasema TRA inawahakikishia wananchi wote kuwa jitihada za ukusanyaji mapato zinaendelea kwa ukamilifu wake ili kufikia lengo la makusanyo katika Mwaka wa Fedha 2025/2026.
Kwa kushirikiana na wananchi, TRA inaamini makusanyo hayo yatafanikishwa kwa uadilifu, uwazi na ufanisi kuwezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na huduma nyingine za kijamii kwa manufaa ya taifa zima.