DODOMA: SERIKALI imetenga Sh bilioni 3 kuanza ujenzi wa awamu ya pili wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini mkoani Mtwara, ambapo ujenzi huo unatarajiwa kuanza Aprili 2025.
Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel amesema hayo leo bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Nanyamba mkoani Mtwara, Abdallah Chikota alilohoji ni lini ujenzi wa awamu ya pili wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini utaanza?
Akijibu swali hilo, Dk Mollel amesema taratibu za kumpata mkandarasi zimeanza hata hivyo zabuni imeshatangazwa na baada ya wiki mbili watakamilisha hatua hiyo.
“Usanifu wa michoro umeshakamilika na tayari taratibu za kumpata mkandarasi zimeanza, huku zabuni ikiwa imeshatangazwa, na ndani ya wiki mbili tutakuwa tumekamilisha hatua hii,” amesema Dk Mollel.
Amsema fedha hizo zitatumika kujenga jengo la mama na mtoto, nyumba za watumishi, kichomea taka, na jengo la kufulia.
Aidha, Dk. Mollel amethibitisha kuwa serikali imejipanga katika kuhakikisha ujenzi huo na utaanza kama ilivyopangwa, ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa mikoa ya kusini.
Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini inatoa huduma za kibingwa kwa wananchi wa mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, na maeneo jirani.