Ujenzi, ukarabati miundombinu ya usafirishaji waimarika

UJENZI, ukarabati na matengenezo ya miundombinu ya barabara na usafi rishaji nchini unazidi kuimarika na kuwawezesha wananchi kuendesha shughuli zao za kijamii na kiuchumi.
Taarifa ya bajeti ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) 2023-2024 inasema kuwa hadi kufikia Machi, 2024 urefu wa barabara zilizojengwa kwa kiwango cha lami umeongezeka kutoka kilometa 2,025 hadi kufikia kilometa 3,224.
Ongezeko hilo ni sawa na asilimia nne ya lengo la ofisi hiyo. Ni kweli kwamba Tamisemi kupitia Tarura imeendelea
kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja nchini kwa kujenga barabara za lami pamoja na zile za changarawe.
Hatua hii imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupitia makusanyo ya fedha za Mfuko Mkuu wa Serikali, tozo za mafuta na fedha za mfuko wa barabara.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo kwa upande wa fedha za Mfuko wa Barabara, barabara zenye urefu wa kilometa 12,417 zilifanyiwa matengenezo ambapo barabara za lami zenye urefu wa kilometa 15 zilijengwa.
Kimsingi katika kuboresha miundombinu tozo za mafuta zilitumika ambapo barabara za lami zenye urefu wa kilometa 90 zilijengwa huku fedha za Mfuko Mkuu wa Serikali zimetumika kujenga barabara za lami zenye urefu wa kilometa 50.
Kwa upande wa barabara za changarawe urefu wa barabara kutoka kilometa 24,493 hadi kilometa 41,107 sawa na asilimia 17 ya lengo.
Aidha, kupitia fedha za Mfuko wa Barabara zilitumika kufanya ukarabati na matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilometa 74 pamoja na wa madaraja 20, makalavati 100 na mifereji ya kuondoa maji barabarani yenye urefu wa meta 50,563.
Kwa upande wa fedha za tozo ya mafuta, fedha hizo zimetumika kujenga barabara za changarawe zenye urefu wa kilometa 2,658 na ujenzi wa mitaro ya maji ya mvua yenye urefu wa meta 8,298.
Fedha za Mfuko Mkuu wa Serikali zimetumika kukarabati na kujenga barabara za changarawe kilometa 1,225 ujenzi wa madaraja 28, makalavati 60 na mifereji ya maji ya mvua yenye urefu wa meta 4,460.
Serikali bado inaendelea na jitihada za kuimarisha miundombinu ya barabara kupitia wakala wa barabara za mijini na vijijini.
Katika kufanikisha hilo hivi karibuni Ofisi ya Rais, Tamisemi kwa kushirikiana na Benki ya CRDB walizindua hatifungani ya miundombinu ya Samia.
Katika uzinduzi huo Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alisema hatifungani hiyo itaiwezesha Tarura kuongeza mtandao wa barabara za vijijini na mijini kwa kuwashirikisha wawekezaji wa ndani katika kugharamia miradi ya miundombinu.
Dk Mpango alisema kuanzishwa kwa hatifungani itawezesha kukuza ushirikiano na Sekta Binafsi na kuhakikisha ujenzi na ukarabati wa barabara zinazosimamiwa na Tarura unafanyika kwa wakati ili barabara hizo ziweze kutumika katika kipindi chote cha mwaka.
Akizungumza katika hafla hiyo Dk Mpango alisema mtandao wa barabara za lami nchini umeongezeka kutoka
kilometa 13,235.1 mwaka 2020 hadi kufikia kilometa 15,366 mwaka 2024.
Aidha, bajeti ya Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini imeendelea kuongezeka kutoka Sh bilioni 414 mwaka 2019/2020 hadi Sh bilioni 841 mwaka 2024/2025.
Dk Mpango alisema hatifungani hii itaiwezesha Tarura kukabiliana na mahitaji ya dharura ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu unaosababishwa na uharibifu wa mvua kubwa zinazonyesha na kusababisha mafuriko.
Ni dhahiri kwamba serikali imeazimia kuboresha ujenzi wa miundombinu ya barabara ili kuchochea maendeleo katika sekta mbalimbali na ndio maana inafanya kila linalowezekana kuboresha miundombinu hiyo.
Taarifa ya hali ya uchumi ya 2023 imeeleza kuwa serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya barabara nchini.
Kwa mujibu wa taarifa ya hali ya uchumi nchini mwaka uliopita zaidi ya kilometa 144,429 za barabara zilisimamiwa na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mjini.