Ujenzi wa barabara ya Iringa, Hifadhi ya Ruaha waiva

WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, ameongoza tukio la kihistoria la kusaini mkataba wa ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 104 inayounganisha Iringa Mjini na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, moja ya vivutio vikubwa vya utalii nchini Tanzania.

Mradi huu, ambao umekuwa ndoto ya wananchi kwa zaidi ya miaka 60, utaanza kutekelezwa kwa gharama ya Sh bilioni 142.56 na kampuni ya China Henan International Company Limited (CHICO) na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 24.

Waziri Bashungwa aliwahakikishia wananchi kuwa fedha za mradi huu zitatolewa bila kukwama, na akaahidi usimamizi thabiti wa ujenzi huu muhimu.

“Fedha zitatiririka tangu siku ya kwanza hadi mradi utakapokamilika. Hakutakuwa na ucheleweshaji au upungufu wowote,” alisema Bashungwa, akiwataka TANROADS kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.

Salim Asas, mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, alitoa pongezi zake kwa serikali kwa kutimiza ahadi ya muda mrefu ya kujenga barabara hiyo akisema, “Nimesoma Ilani zote, na kila mara barabara hii ilikuwa ikitajwa. Sasa Rais Samia ameweka historia kwa kutekeleza mradi huu mkubwa.”

Mbunge wa Kalenga, Jackson Kiswaga, alitumia fursa hiyo kujinadi kwa uchaguzi wa 2025, akisema, “Ujenzi wa barabara hii ni ushindi mkubwa kwa wapiga kura wangu wa Kalenga. Nina matumaini mtanichagua tena kwa asilimia 90,” alisema huku akisisitiza kuwa ni ndoto ya muda mrefu kwa mkoa wa Iringa.

Naye Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Jesca Msambatavangu, alisema kuwa barabara hiyo itakuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya mkoa wa Iringa, hasa kwa kuongeza ajira na kuimarisha sekta ya utalii wa kusini.

Mbunge wa viti maalumu wa Mkoa wa Iringa, Nancy Nyalusi, alisema, “Ujenzi wa barabara hii utafungua njia na fursa nyingi za kiuchumi, utalii, na maendeleo ya kijamii kwa mkoa wa Iringa na kanda ya kusini kwa ujumla.”

Rose Tweve, Mbunge wa Viti Maalumu, aliwataka vijana kuweka akiba na kutumia barabara hiyo ipasavyo kwa maendeleo yao ya kiuchumi.

“Vijana wajipange ili barabara hii iwe fursa kwao ya kujiendeleza kiuchumi,” alisema Tweve.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Pindi Chana, alisisitiza umuhimu wa barabara hiyo katika kukuza utalii wa kusini akisema itaongeza idadi ya watalii na kukuza sekta ya utalii ambayo huchangia asilimia 17 ya Pato la Taifa lakini pia itaharakisha uwekezaji katika maeneo ya kimkakati ndani ya hifadhi.

Kwa upande wake, Mbunge wa Isimani, William Lukuvi, alifurahia hatua ya ujenzi wa barabara hii, akisema, “Ndoto ya kujenga barabara ya lami inayounganisha Hifadhi ya Ruaha ni ya muda mrefu. Hatimaye imekuja kutimia katika awamu ya sita.”

Aliongeza kuwa atahamia kijijini kwake Idodi baada ya kukamilika kwa barabara hiyo, akisisitiza umuhimu wa mradi huo kwa maendeleo ya vijiji vinavyopakana na hifadhi hiyo.

Meya wa Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada, aliwashukuru viongozi kwa juhudi zao za kufanikisha mradi huo akisema barabara hiyo ni matokeo ya juhudi za miaka mingi, na akashukuru kuona utekelezaji wake unakwenda kuanza.

Wakati huo huo, Waziri Bashungwa aliwahakikishia wananchi watakaopisha mradi huo kuwa fidia itatolewa kwa wale wanaostahili.

“Asijitokeze mtu yeyote akawapotosha. Serikali imejipanga, na wale wanaostahili fidia watapata malipo yao,” alisisitiza Bashungwa.

Habari Zifananazo

Back to top button