Ukatili wowote udhibitiwe shuleni ili wanafunzi wasome kwa amani

SHULE za msingi na sekondari zinafunguliwa leo nchi nzima ikiwa ni muhula wa kwanza wa masomo kwa mwaka 2026.

Wiki moja iliyopita, wanafunzi walioandikishwa kuanza elimu ya awali, msingi na kidato cha kwanza, walifungua shule wao kwanza ili kuwajenga kisaikolojia kuzoea mazingira ya shule, kujua taratibu za shule kabla shule nzima hazijafunguliwa.

Hatua hii ni nzuri kwani inasaidia kwa kiasi kikubwa wanafunzi hao ambao madarasa wanaoingia ni mapya kwao, kuelewa taratibu, mazingira na kuwasaidia kuwa wenyeji kabla ya wenzao.

Hata hivyo uzoefu unaonesha wanafunzi wa madarasa mapya hupata usumbufu kutoka kwa wanafunzi wenzao wa madarasa ya juu na hivyo kuwafanya kuichukia shule na elimu ikiwa hawatasaidia kuzuia hali hizo shuleni.

Wapo baadhi ya wanafunzi wa madarasa ya juu huwasumbua kwa kuwatania na kuwaita majina mabaya, kuwatuma kazi ngumu kwa lazima na wanapokataa huwapiga au kuwatuma vitu kwa lugha za kisayansi wakijua hivyo ni vifaa vya maabara na si vitu vya kununuliwa hovyo hovyo.

Kuna baadhi pia ya walimu huwanyanyasa kisaikolojia wanafunzi hawa wapya katika madarasa yao ama kwa kuwapiga isivyo kawaida, kuwapa adhabu nyingi, kuwatuma hata muda wa vipindi, kuwakemea kwa maneno mabaya mbele ya wenzao hali inayowaumiza na kuchangia kufanya vibaya katika masomo.

Tunafahamu kuna watoto kwa asili ni wakorofi kutokana na malezi au tabia za kurithi, lakini mambo haya yasiwe sababu ya kumfanya mwanafunzi atendewe vitendo vibaya vya kumfanya achukie shule au kusoma.

Tunawakumbusha wanafunzi wa madarasa ya juu kuwachukulia wanafunzi hawa wageni kama wadogo zao, kuwapenda na kuwafundisha kwa upole nidhamu na mazingira ya shule ikiwa ni pamoja na kuwaelekeza kanuni na taratibu za kufuata kwa kila shule ilivyojiwekea.

Walimu na wazazi katika hili wawe mstari wa mbele kuhakikisha wanafunzi hawa wanapenda mazingira ya shule na wanakuwa na utulivu na amani ili wafikie ndoto zao.

Tukumbuke Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imewekeza Sh trilioni 2.439 katika bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia mwaka 2025/2026 na imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya elimu kumuwezesha kila mtoto wa Kitanzania kusoma.

Shule zimejengwa na zinaendelea kujengwa, ajira za walimu zinaendelea kutoka, mazingira rafiki ya elimu shule za msingi na sekondari yanaendelea kuboreshwa, tutumie fursa hii kuwapa raha wanafunzi kusoma kwa amani na utulivu dhidi ya ukatili wa namna yoyote shuleni.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button