Ulega aiongoza Wizara kuwafariji Hanang
MANYARA: Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amefika wilayani Hanang, mkoani Manyara kwa lengo la kutoa pole na kukabidhi mchango wa wadau na wizara kwa wananchi walioathirika na mafuriko wilayani humo.
Wakati akitoa salamu hizo za pole Desemba 11, 2023, Ulega amesema kuwa wizara yake imepokea kwa masikitiko makubwa tukio la mafuriko hayo yaliyotokea na kusababisha kupotea kwa maisha ya Watanzania pamoja na uharibifu wa mali na mifugo.
Aidha,Ameeleza kuwa kufuatia kadhia hiyo, wizara yake kwa kushirikiana na wadau katika sekta ya mifugo na uvuvi wakiwemo ASAS, Bajuta International, Dalberg International, Karie Kinana, APOKA, TAFMA, TABROFA na TPBA) kwa pamoja wameandaa vitu mbalimbali na kuvikabidhi kwa Kamati ya Maafa ya Kitaifa kwa ajili ya uratibu wa namna nzuri ya kuvifikisha kwa familia na walengwa wote.
Miongoni mwa vitu hivyo ambavyo amevikabidhi ni pamoja na Ng’ombe 13, Mbuzi 20, Trei 90 za mayai, Fedha tasilimu jumla ya Sh milioni 5, Maziwa katoni 300, Sembe, Maharage na Chumvi.
“Kufuatia tukio hili lililoumiza mioyo ya watanzania wote, wizara yangu inaungana na Rais, Samia Suluhu Hassan kutoa pole kwa familia zote zilizopatwa na matatizo”, alisema
Pia, amebainisha kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi itaendelea kushirikiana na Kamati ya Taifa ya Maafa na Uongozi wa mkoa na wilaya ili kubaini uharibifu wote wa miundombinu ya mifugo na kuirejesha katika hali yake kwa haraka ili kuhakikisha mifugo inaendelea kupata huduma stahiki na kuwezesha wafugaji kunufaika na mifugo yao kwa maendeleo ya nchi.
Waziri Ulega amesisitiza kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Dk.
Samia Suluhu Hassan itaendelea kusimama na watanzania wote katika hali zote ambazo zinawapata watanzania akiongeza kuwa wao kama wasaidizi wake wapo imara kuhakikisha adhma yake ya kuendelea kuwaletea maendeleo Watanzania inatimia.
Waziri Ulega amekabidhi vifaa hivyo kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama kwa niaba ya waathirika wa mafuriko hayo.