Ulinzi yajivunia usalama miradi, ujenzi wa uchumi

WIZARA ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imesema inajivunia mafanikio katika miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, ikiwemo usalama wa miradi ya kimkakati na kuchangia kujenga uchumi.

Pia, bajeti ya wizara hiyo imeongezeka kutoka Sh trilioni 2 mwaka 2021/22 hadi kufikia Sh trilioni 3.6 mwaka wa fedha 2025/26 na huduma za afya zikiimarishwa na asilimia 80 ya wanufaika wa huduma hizo ni raia.

Waziri wa wizara hiyo, Dk Stergomena Tax amesema hayo Dodoma wakati akieleza mafanikio katika kipindi cha miaka minne.

Dk Tax pia mafanikio katika Sekta ya Ulinzi ni ujenzi na ulinzi wa miradi ya kimkakati ikiwamo Ujenzi wa Ikulu Chamwino, ulinzi wa Reli ya Kisasa (SGR), ulinzi wa mradi wa kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere, ulinzi wa mgodi wa Tanzanite, bandari, viwanja vya ndege na uundaji wa meli katika Ziwa Victoria.

Alisema kupitia SUMAJKT imechangia katika ujenzi wa uchumi ili kuipunguzia serikali gharama za uendeshaji wa mafunzo kwa vijana wa JKT.

Dk Tax pia, alisema wizara hiyo kupitia JKT imetekeleza mkakati wa kilimo unaolenga kuongeza uzalishaji wa mazao na kujitosheleza kwa chakula ili kuipunguzia serikali gharama za kulisha vijana wanaohudhuria mafunzo ya JKT na kuchangia katika usalama wa chakula wa taifa.

Alisema serikali kupitia wizara hiyo imehakikisha tunu muhimu za taifa yaani amani, ulinzi na usalama zinalindwa kwa kuimarisha umoja, mshikamano na utulivu nchini.

Alisema pia, wizara hiyo kupitia JWTZ imeendelea kulinda amani, kulinda mipaka ya Tanzania na kuhakikisha mipaka inakuwa salama na kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya vitendo vyote vyenye viashiria vya uvunjifu wa amani.

Dk Tax alisema wizara hiyo kupitia JKT imetoa mafunzo kwa vijana 143,863 wa mujibu na vijana wa kujitolea 46,196, mafunzo ambayo yamewajengea vijana maadili mema, uzalendo, ukakamavu, umoja wa kitaifa na kuwapatia stadi za kazi na uhodari katika nyanja mbalimbali.

Alisema pia, imetoa mafunzo ya mgambo kwa vijana 55,790 wa Kitanzania katika mikoa yote ya Tanzania ikiwa ni sehemu ya Jeshi la Akiba.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button