Umeme vijijini wakamilika, vitongoji wafikia 50%

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko.

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema mafanikio ya kufikisha umeme kwa asilimia 100 vijijini yametokana na maono ya Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta ya nishati.

Akizungumza kwenye kipindi cha Dakika 45 cha ITV, Dk Biteko ameeleza kuwa serikali sasa imeanza kufikisha umeme kwenye vitongoji baada ya kukamilisha kufikisha huduma hiyo katika vijiji 12,318 nchini.

“Vijiji karibu asilimia 100 vimefikiwa na umeme, na sasa tunakwenda kwenye vitongoji. Kati ya vitongoji 64,000, tayari vitongoji 34,000 vimepata umeme,” amesema.

Advertisement

Dk Biteko amefafanua kuwa sekta ya nishati imepiga hatua kubwa, tofauti na miaka ya nyuma.

Amesema kwa sasa, mitambo ya kuzalisha umeme ina uwezo wa kuzalisha megawati 3,071, wakati mahitaji ya juu ni megawati 1,888.

Amesema hali hii imeifanya Tanzania kuwa na ziada ya umeme inayoweza kuuzwa kwa nchi jirani.

Kwa mujibu wa Dk Biteko, maendeleo hayo yameongeza matumizi ya umeme katika miradi mikubwa, ikiwemo reli ya kisasa ya SGR na migodi mikubwa kama Geita Gold Mine, ambayo sasa imeunganishwa na gridi ya taifa.

Amesema serikali pia, imekuwa ikiboresha miundombinu ya kusafirishia umeme ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka.

“Miundombinu mingi iliyopo ni ya zamani. Tunabadilisha transfoma ndogo na kuweka kubwa, kupanua vituo vya kupoza umeme na kuboresha njia za kusafirisha umeme,” amesema.

Aidha, amesema serikali inaendelea kuunganisha mikoa ya Lindi, Mtwara na Katavi na gridi ya taifa ili kuhakikisha
mikoa hiyo pia, inapata umeme wa uhakika.

Kuhusu kukatika kwa umeme, Dk Biteko amesema mfumo mzuri wa kuratibu taarifa umeanzishwa kupitia mameneja wa wilaya na mikoa.

“Muda mwingine umeme hukatwa kwa matengenezo. Ni lazima tukubali hali hiyo ili kuepusha matatizo makubwa zaidi,” amesisitiza.

Pia, amegusia mafanikio ya Tanzania katika sekta ya nishati, ambayo yameifanya nchi kuwa mwenyeji wa mkutano wa kimataifa.

“Mwaka 2014 upatikanaji wa umeme ulikuwa asilimia 42, lakini sasa tupo asilimia 78. Tanzania inatajwa kama
mfano wa mafanikio,” ameisema.

Amewasihi wananchi kutumia fursa zinazotokana na mkutano huo kwa shughuli halali kama biashara, utalii, na usafiri, ili kuongeza kipato.