Umuhimu wa maboresho ya kodi katika ukuaji soko la hisa
MABORESHO ya kodi ni jambo muhimu katika kubadili hali ya uchumi kwa kuwa yanagusa moja kwa moja sekta
mbalimbali, likiwamo soko la hisa. Nchini Tanzania, Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) ndilo jukwaa kuu ambapo
maboresho haya ya kodi yanadhihirika.
Kwa mujibu wa maoni yaliyokusanywa na gazeti la DailyNews kutoka kwa wataalamu wa soko la hisa, maboresho ya sera za kodi yanaweza kuathiri imani ya wawekezaji, kiasi cha biashara na kuathiri soko lenyewe kwa namna mbalimbali.
Yafuatayo ni maoni yaliyotolewa na watalaamu hao kuhusu suala hili pamoja na maeneo yanayohitaji kuboreshwa ili
kuunda mfumo bora wa kodi kwa ukuaji endelevu wa nchi. Meneja wa Utafiti na Uchambuzi wa Vertex International Securities, Beatus Mlingi anasema,
“Kwa kiasi kikubwa maboresho ya kodi huathiri uamuzi katika uwekezaji, huathiri mzunguko wa mtaji na pia, huathiri shughuli za soko.” Anaongeza: “masoko ya hisa, kama kipimo cha uhai wa uchumi yanastawi katika mazingira yanayohamasisha uwekezaji”.
Makala haya yanajikita kuangalia uhusiano uliopo kati ya maboresho ya kodi na masoko ya hisa hasa kwa kuzingatia DSE. Kuchanganua mfumo wa kodi uliopo sasa na kupendekeza maboresho ya kimkakati, kunalenga kuonesha namna mfumo bora wa kodi unavyoongeza shughuli za soko na kuchochea ukuaji wa uchumi.
MABORESHO YA KODI KUENDELEZA SOKO LA HISA
Maboresho ya kodi yanaweza kuchochea ukuaji wa soko kwa kupunguza gharama za miamala, kukuza imani ya wawekezaji na kuongeza ukwasi wa soko. Mara nyingi nchi zinazotoa faida ya kodi huvutia uwekezaji zaidi ama uwe wa ndani au wa kigeni.
Sera kama vile kupunguzwa kwa kodi ya faida ya mitaji, motisha katika kodi za mashirika yaliyoorodheshwa na taratibu rahisi za kodi huchochea ushiriki wa kina katika soko na kuchochea uwekezaji wa muda mrefu.
Kinyume chake, kiwango kikubwa cha kodi kinaweza kufifisha shughuli za soko, kupunguza kiwango cha biashara na kuzuia uwekezaji. Mazingira ya kodi yanayowiana ni muhimu katika kusaidia ukuaji wa soko la hisa na utulivu wa uchumi kwa ujumla.
Kwa mfano, kuwekewa kwa kiwango kikubwa katika kodi za miamala ya kifedha, kwa kiasi kikubwa kunaweza
kuzuia mzunguko wa mtaji. Kwa upande mwingine, kuanzishwa kwa sera rafiki za biashara na uwekezaji kunaweza kuhamasisha wawekezaji kufanya uamuzi makini, hivyo kuongeza shughuli za soko na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Kimsingi, athari za mfumo imara wa kodi kwa maendeleo ya soko la hisa hazipaswi kupuuzwa. Hali hii huchochea uwekezaji wa namna mbalimbali, hivyo kuvutia washiriki wa ndani ya nchi na hata wa kigeni. Kwa Watanzania, mfumo shindani wa kodi katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) pia unaweza kuanzisha utamaduni wa kuokoa na kuwekeza katika soko, hivyo kuongeza utajiri.
KODI NA ATHARI ZAKE ZA SASA KWA DSE
Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) lina nafasi kubwa katika uanzishwaji na uunganishwaji wa mtaji, biashara na wawekezaji. Hata hivyo, ukuaji huo wa soko unakwamishwa na mfumo wa kodi ambao licha ya kuwa muhimu kwa ukusanyaji wa mapato, unadhibiti shughuli za soko.
Sera muhimu za kodi zinazotekelezwa sasa zinaathiri mwenendo wa wawekezaji, ukwasi wa soko na ushindani.
Kodi ya asilimia 10 ya ongezeko la mtaji kutoka katika biashara ya dhamana, ingawa ni ya wastani ikilinganishwa na
viwango vya kimataifa, inazuia biashara ya kubahatisha ambayo ni kipengele muhimu kuongeza ukwasi wa soko.
Mfumo wa kodi wenye ufanisi zaidi unaweza kuhamasisha kiwango kikubwa cha biashara na hata kunufaisha
wawekezaji na soko kwa ujumla. Punguzo la kodi ya faida ya mtaji litanufaisha wafanyabiashara wa muda mfupi
ambao huongeza ukwasi katika soko, hivyo kuwezesha kasi ya mzunguko wa mtaji.
Hali hii huwezesha ongezeko la mapato kwa serikali na kwa wawekezaji binafsi. Aidha, asilimia 10 ya kodi ya zuio katika gawio hupunguza faida halisi kwa wawekezaji, hasa wa kigeni. Gharama hizi za ziada hupunguza ushindani wa DSE ikilinganishwa na masoko ya kikanda.
Maboresho katika sera hii ya kodi yanaweza kuvutia mtaji wa kimataifa, kuongeza ukwasi wa soko na kukuza hadhi ya DSE kama kitovu cha soko la hisa katika kanda. Kimsingi wawekezaji mara nyingi hutathmini utaratibu wa kodi kwa gawio wanapochagua mahali pa kuwekeza. Kodi nafuu inaweza kufanya DSE kuwa chaguo bora.
Wakati kampuni zilizoorodheshwa zinanufaika na kiwango cha chini cha kodi za mashirika, kukosekana kwa ufahamu kuhusu manufaa haya kunapunguza umuhimu wake. Kuongeza ufahamu kuhusu manufaa haya kutahamasisha kampuni/mashirika zaidi kujiorodhesha katika DSE, hivyo kuongeza nafasi za uwekezaji na kusaidia
soko kufikia malengo ya ukuaji.
Motisha za kodi kwa mashirika zinaweza kupanuliwa ili kujumuisha tasnia zinazochipukia kama vile teknolojia na nishati jadidifu kuvutia wawekezaji na wajasiriamali. Kimsingi, gharama kubwa za miamala hasa katika ada za
mawakala wa hisa huathiri zaidi wawekezaji wa rejareja (binafsi).
Kupunguza gharama hizi au kutoa motisha kama vile akaunti zisizo na kodi kwa wawekezaji wa rejareja kunaweza kuongeza ushiriki zaidi wa soko na kuchochea utamaduni wa uwekezaji. Wawekezaji wengi wa rejareja
wakiingia sokoni, DSE itashuhudia ongezeko la ukwasi wa soko na aina mbalimbali dhamana za kibishara.
ATHARI ZINAZOWEZA KUTOKANA NA MABORESHO YA KODI DSE
Maboresho yanayolengwa katika kodi yanaweza kuimarisha utendaji na mvuto wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) na kufungua fursa za ukuaji na kuchangia katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania. Kupunguza au
kuondoa kodi ya ongezeko la mtajikatika biashara kunaweza kuongeza kiasi cha biashara ya muda mfupi na
kuvutia washiriki zaidi.
Kupunguza kodi ya zuio ya gawio kwa wawekezaji wa kigeni kutafanya DSE kuwa na ushindani zaidi katika kanda, na kuvutia mitaji ya kimataifa na ujuzi wa kimataifa. Hii itasaidia kukuza soko lenye ukwasi zaidi na kuimarisha uhusiano kati ya kampuni za Tanzania na wawekezaji wa kimataifa.
Kuingiza motisha za kodi kwa wawekezaji wa muda mrefu kutasaidia kudumisha uimara wa soko na kuvutia uwekezaji wa kimkakati. Wawekezaji wenye hisa za muda mrefu hutoa uthabiti unaohitajika katika kukabiliana na mabadiliko ya soko.
Kwa kutoa motisha kama vile kupunguza viwango vya kodi kwa hisa za muda mrefu, Tanzania itavutia wawekezaji
wa kitaasisi wenye uwezo wa kuhimili maboresho ya soko.
Aidha, kupunguza kodi kwa wawekezaji wa rejareja (watu binafsi) kutakuza ushiriki na kuimarisha ustahimilivu wa soko. Ongezeko la motisha katika kodi za mashirika litahamasisha biashara na mashirika kujitokeza zaidi kujiorodhesha DSE.
Litaongeza pia fursa za uwekezaji na kuimarisha nafasi ya soko kuhamasisha mitaji. Kwa kuongeza mashirika yaliyoorodheshwa kutoka katika biashara ndogo na za kati (SMEs) hadi mashirika makubwa ya kimataifa, Tanzania itavutia wawekezaji.
Hatimaye, kutoa misamaha ya kodi kwa miamala ya kidijiti kutavutia wawekezaji mpya wenye ujuzi wa teknolojia sambamba na mwenendo wa biashara za kisasa za hisa na kufanya soko kuwa jumuisha zaidi. Urahisi huu kufikia majukwaa ya kidijiti pamoja na motisha katika kodi utavutia kizazi cha wawekezaji kilichozoea biashara mtandaoni
na programu tumizi za kidijiti.
MIFANO YA MABORESHO YA KODI KATIKA MASOKO MENGINE
Maboreshoya kodi yamedhihirika kuwa chachu ya ukuaji wa masoko duniani. Nchini India, maboresho hayo yaliyowapa motisha wenye hisa za muda mrefu, huku yakipunguza kodi ya ongezeko la mtajiza muda mfupi, yalisaidia kuimarisha soko. Hatua hizo zilivutia wawekezaji wa kitaasisi na wa rejareja.
Huko Singapore, msamaha waongezeko la mtaji na motisha kwa kampuni na mashirika kuorodheshwa umewawezesha kuwa kitovu cha kifedha duniani. Gharama za chini za miamala na mifumo ya kodi
iliyorahisishwa zimeongeza ushindani wa soko na kuvutia uwekezaji wa kimataifa.
Kwa kuweka mazingira rafiki kwa mashirika na wawekezaji, Singapore imejijenga kama kiongozi katika masoko ya kifedha wa kikanda. Nchini Kenya, kuondolewa kwa muda kwa kodi ya ongezeko la mtaji mwanzoni mwa miaka ya 2000 kulisababisha ongezeko kubwa la shughuli za biashara katika Soko la Hisa la Nairobi (NSE) na kuonesha
namna sera ya kodi inavyoweza kuchochea uhai wa soko.
Hatua hiyo iliongeza imani ya wawekezaji, ikakuza ukwasi wa soko na kuongeza wawekezaji wa soko.
MAPENDEKEZO YA MABORESHO YA KODI TANZANIA
Tanzania inaweza kunufaika kupitia mapitio ya kodi ya ongezeko la mtaji na kutoa misamaha kwa faida zinazorejeshwa. Utekelezaji wa akaunti zisizo na kodi kama vile Akaunti za Akiba za Binafsi za Uingereza, utahamasisha ushiriki wa muda mrefu kwa wawekezaji binafsi.
Hali hii itawawezesha wawekezaji kukusanya utajiri kwa muda na kuhakikisha faida zao haziathiriwi na kodi.
Ili kuhamasisha mashirika zaidi kujiorodhesha DSE, punguzo zaidi la kodi linaweza kutolewa kwa mashirika yanayokidhi vigezo kama vile kuunda ajira au kufikia malengo ya kimazingira, kijamii na kutawala.
Aidha, kurahisisha utekelezaji wa sheria za kodi kwa watu binafsi na wawekezaji wa taasisi kutapunguza vikwazo vya kiutawala na kufanya DSE kuwa kivutio zaidi cha uwekezaji. Kwa kupunguza ugumu katika taarifa za kodi, Tanzania itakuza imani ya wawekezaji na kuchochea ushiriki zaidi katika soko la hisa.
Elimu kwa umma ni muhimu ili kuhakikisha wawekezaji na mashairika wanatambua na kutumia motisha hizi za kodi. Kwa kuelimisha wadau, serikali na mamlaka zinazohusika na udhibiti zinaweza kuhamasisha ushiriki mpana na kuongeza athari chanya za maboresho.
Kufikia umma kupitia njia za kidijiti, semina na warsha kutasaidia kuelimisha umma kuhusu masoko ya hisa na sera za kodi, kuongeza wawekezaji na kukuza uelewa kuhusu uchumi. Hatimaye, kulinganisha sera za kodi za Tanzania na nchi jirani kutasaidia kuhakikisha DSE inabaki kuwa mshindani imara ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ikichochea ukuaji na ushirikiano wa kikanda.
Kwa kuoanisha sera za kodi na viwango vya kimataifa, Tanzania itajiweka katika nafasi ya kuwa kivutio kikubwa zaidi cha uwekezaji katika soko la Afrika.
HITIMISHO
Maboresho ya kodi yana nafasi na uwezo mkubwa wa kuchochea ukuaji wa DSE na kuchangia maendeleo ya uchumi
wa Tanzania.



