Umuhimu wa vijana kujengewa uwezo katika siasa

“VIJANA wasiseme siasa haiwahusu, wajue kila mmoja siasa inamuhusu hata kama hujihusishi nayo.”

Ndivyo anavyosema Ofisa Mradi na Mtafiti wa Taasisi ya Tanzania Youth Vision Association (TYVA), Athuman Msangi na kuongeza: “Tunatoa mwito kwa vijana kutoa sauti zao kupitia upigaji kura ili kupata Tanzania bora zaidi.”

Kwa mujibu wa Msangi, siasa ndio inayoamua maisha hasa uchumi wa vijana kama vile mazingira ya ufanyaji kazi zikiwamo za biashara, kilimo, ufugaji na nyingine hivyo hawapaswi na hawawezi kukwepa siasa.

Anawashauri kushiriki kikamifu katika mchakato wa siasa, uchaguzi na uongozi kwani kwa namna yoyote mambo hayo hugusa na kuathiri maisha yao. Katika kuhakikisha vijana wanapata uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya siasa, taasisi hiyo kwa kushirikiana na shirika la Forum Civ imetekeleza mradi unaoitwa Strength Agency for Social
Accountability (SASA).

Mradi huo ulioanza mwaka 2024 unalenga kuwajengea uwezo vijana katika eneo la elimu ya uraia hususani kushiriki katika mchakato wa uchaguzi. Hii ni pamoja na kugombea ili kuchaguliwa kuwa kiongozi na kupiga kura kuchagua viongozi wengine. Elimu hiyo ilitolewa katika mikutano ya mitandao ya kijamii na mafunzo ya ana kwa ana na kuwafikia vijana 70,000 nchini.

“Sasa tumefanya tathmini kuangalia kama elimu tuliyoitoa imefanikiwa hasa kwa wale waliofanikiwa kushiriki
uchaguzi kwa kugombea na kupiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Mwaka 2024,” anasema.

Kwa mujibu wa Msangi, wamefanya tathmini katika kata mbili kwa wilaya tano za Mkoa wa Dar es Salaam na kila kata walihoji watu 10 na vijana waliogombea, walioshindwa na walioshinda ili kujua changamoto zao.

“Tumefanya tathmini kwa vijana 110 katika Mkoa wa Dar es Salaam. Tulianza tathmini Januari 2024 na mafunzo tulianza Mwezi wa Tatu hadi Mwezi wa Saba 2024. Tuliwafikia vijana 100 ana kwa ana na mitandaoni tumefikia vijana 70,000,” anafafanua.

Anaongeza: “Tumeona namna vyama vya siasa vinavyotengeneza vijana kuwa viongozi, pia jinsi walivyotumia mitandao ya kijamii kufanya kampeni vikiwemo vikundi sogozi katika WhatsApp na mitandao mingine ambayo gharama zake ni nafuu zaidi”.

Anasema miongoni mwa changamoto walizokuta kwa vijana ni mwamko mdogo wa kushiriki katika shughuli za siasa na wengine kuhama katika maeneo ya vituo walivyojiandikisha. Aidha, wamezungumzia suala la rushwa ya ngono hasa dhidi ya vijana wa kike.

Mapendekezo ya Vijana
Mtafiti, Erickson Duke anasema katika kutoa elimu wamewashirikisha vijana wa kike na kuwafanya midahalo na kuwakutanisha na wanasiasa wa kike waliofanikiwa. Duke anasema miongoni mwa mapendekezo ya vijana ni uhitaji
wa vyombo huru vya uchaguzi na vya haki vitakavyofanya uamuzi wa haki katika uchaguzi.

Kwa sasa shughuli za Uchaguzi Mkuu Tanzania zinaandaliwa na kusimamiwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi
(INEC). “Wamesema elimu ya uraia ipewe kipaumbele ili kutoa motisha kwa vijana kuwa na mwamko zaidi kwa kuondoa mawazo kuwa wazee pekee ndio wanastahili kugombea.

Anaongeza: “Vijana wamelalamika kutopata nafasi nakwamba sura za uchaguzi kila siku hazibadiliki huku kukiwa hakuna mabadiliko katika jamii, hivyo kupata nafasi kwao inakuwa ni vigumu na wao kubakiwa tu, na jukumu la kupiga kura.”

Anasema vijana walisema upigaji kura kidijiti utarahisisha kura kuhesabika na kurahisisha gharama sambamba na kuendana na sayansi na teknolojia.

“Wanasema hii itatengeneza mwanya wa uchaguzi kuaminika zaidi na itakuwa rahisi kwa vijana na itawafanya vijana kuleta mawazo mapya na nguvu mpya na kujiunga na vyama vya kisiasa na kujiamini wanaposhirikiana,” anafafanua.

Mtafiti mwingine, Halfan Ismail anasema vijana wasipoona mabadiliko hukata tama. Kwa mujibu wa Ismail, vijana
wanapendekeza huduma za kijamii ziboreshwe na kipato chao kiimarishwe ili kuwapa nguvu zaidi kushiriki katika siasa wakiwa na utulivu.

“Miongoni mwa mapendekezo waliyopata kutoka kwa vijana ni uwepo wa elimu zaidi ya uraia katika maeneo ya vijijini kwa sababu bado wanawake na vijana hawana nafasi nyingi za kugombea,” anasema. Anasema vijana wameshauri upigaji kura kidijiti na kwamba kutasaidia kuweka uwazi zaidi.

Vijana wafunguka walivyoshinda
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Maweni, Kata ya Mji Mwema, Dar es Salaam, Said Mziwanda anasema haikuwa rahisi kwake kama kijana kueleweka kwa kuwa nafasi hiyo ina kazi kubwa ya kutumikia wananchi katika mambo
mbalimbali ukiwamo utatuzi wa migogoro.

Anasema kwa kiasi kikubwa vijana walimuunga mkono kwa kumpigia kura na kwamba, wako tayari kufanya kazi pamoja naye. “Mimi nilitokea UVCCM Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi) na nilijengewa uwezo… Unapita kwenye mchakato wa chama, ilikuwa ngumu wazee kuniamiamini,” anasema.

Anafafanua: “Mbinu niliyotumia kuaminika ni kuwa mfuatiliaji wa miradi kwa kujitolea, wananchi wakaniamini nilijitoa asilimia 100 kwa jamii kwani kunichagua ni lazima nirudishe hizi fadhila kwao,” anasema Mziwanda.

Mjumbe wa Mtaa wa Nyambwela, Kata ya Tandika wilayani Temeke, Dar es Salaam kupitia chama cha ACT-Wazalendo, Zuhura Abdallah anasema alijengewa uwezo kwa kupewa mafunzo kutoka ndani ya chama na mashirika mbalimbali.

“Ili kupita nilipendekezwa, chama kilinipeleka kusomea mambo ya siasa na nikamaliza, walinijengea uwezo na ndani ya chama kuna mafunzo ya siasa, imenijengea ujasiri na uwezo wa kusimama na kuomba kura na jamii imenipokea vizuri, nimechaguliwa kwa kura 648,” anasema.

Kwa msingi huo, wadau mbalimbali wanapendekeza na kusisitiza vijana kujengewa uwezo zaidi ili washiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi wa kisiasa kwa kujitokeza zaidi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na pia, kushiriki katika mikutano ya kampeni na hata siku ya uchaguzi wajitokeze kupiga kura.

Wafanye hivyo wakilenga kuhakikisha kura zao haziharibiki na wala hawatoi mchango wowote kuvuruga au kukwamisha ufanisi wa uchaguzi husika.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button