UNESCO watangaza raha kwa vijana
DAR ES SALAAM: SHIRIKA la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) limesema ipo haja ya kuwekeza kwa vijana kwa kuwapa ujuzi, maarifa na fursa jambo litakalochangia kusukuma maendeleo yao na taifa kwa ujumla.
Mkurugenzi Mkazi wa shirika hilo nchini, Michel Toto amesema hayo Dar es Salaam katika shule ya Aga Khan, ikiwa ni muendelezo wa maadhimisho ya siku ya Umoja wa Mataifa (UN).
Amesema kutoa elimu bora na kwa vijana, kukuza ajira na kuweka mazingira ambayo sauti zao zinasikika na mawazo kuthaminiwa pia ni muhimu katika kuhakikisha uendelevu kwa kundi hilo.
“Tunaadhimisha siku ya UN sio tu kutambua kazi zake bali pia kusherehekea ushirikiano wa kudumu kati ya Umoja wa Mataifa na watu wa Tanzania. Ushirikiano huu ni ushuhuda wa maadili ya pamoja na malengo ya pamoja ambayo yanatuunganisha katika kutafuta usawa zaidi na ulimwengu endelevu,” amesema Toto.
Amesema kauli mbiu ya kimataifa ya maadhimisho ni kuwekeza katika kesho ikisisitiza umuhimu wa kuwaandaa vijana ambao ni viongozi wa kesho kwa changamoto na fursa zilizopo mbele yao na kwamba idadi ya watu sio tu siku zijazo bali pia nguvu inayosukuma maendeleo ya mataifa.
Toto amesema kupitia shule ya Aga Khan wakishirikiana na wadau mbalimbali wanajitolea kuendelea kuisaidia Tanzania katika jitihada zake za kuwekeza kwa vijana.
“Tunafanya kazi kwa pamoja kuweka mazingira yanayoruhusu uvumbuzi, ujasiriamali katika kuwajumuisha vijana hata kwenye kufanya maamuzi yanayoweza kuleta tija kwa maisha yao na ndoto zao,” amesema Toto akimwakilisha Mratibu Mkazi wa UN, Zlatan Milisic.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Elimu ya Aga Khan, Dk Shelina Walli amesema kwa kuadhimisha siku ya umoja wa mataifa inasaidia elimu inayotolewa kwa wanafunzi kuendeleza usawa na uvumilivu kama vitu vinavyotakiwa kuonwa kwa jamii.
Amesema wanafunzi ni viongozi wa kesho na wanahitaji kuona maisha yanavyoweza kuendelea kwa upendo amani na haki za binadamu wote.
Mwanafunzi wa shule hiyo, Grayson Mndeme amesema siku ya UN huzungumzia umoja uwazi na ushirikiano kama dunia, na kama ambavyo dunia ya leo kuna utandawazi inasaidia kuwa pamoja kujiendeleza na kujenga tabia ya kusaidiana.



