Upelelezi kesi ya ‘Dk Manguruwe’ waendelea

UPELELEZI wa kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mkurugenzi na mwanzilishi wa Kampuni ya Vanilla International Limited, Simon Mkondya maarufu kama ‘Dk Manguruwe’ na mwenzake bado unaendelea.

Wakili wa Serikali, Winiwa Kasala alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati kesi hiyo ilipotajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Anna Magutu.

Kutokana na hali hiyo, wakili huyo aliiomba mahakama ipange tarehe nyingine ya kutajwa. Kesi hiyo itatajwa tena Aprili 8, mwaka huu.

Mshitakiwa mwingine katika kesi hiyo ni Mkaguzi wa kampuni, Rweyemamu John. Washitakiwa wote wapo mahabusu.

Katika kesi hiyo, washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka 28, yakiwemo ya kujipatia zaidi ya Sh milioni 90 kwa udanganyifu na utakatishaji, kwa kununua viwanja tisa eneo la Idunda, Mkoa wa Njombe.

Ilidaiwa kuwa washitakiwa hao walitenda makosa hayo katika tarehe tofauti kati ya Januari mosi, 2020 na Desemba mosi 2023 ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam

Iliendelea kudai kuwa mashitaka 19 ni ya kufanya biashara ya upatu katika kipindi hicho, Mkondya akiwa mkurugenzi na John akiwa mfanyakazi wa kampuni.

Inadaiwa kwamba walifanya biashara ya upatu kwa kuwaahidi watu kupata faida mara mbili hadi tatu kulingana na kiasi cha fedha watakazotoa.

Iliendelea kudai kwamba washitakiwa hao walijipatia Sh milioni 92.2 kutoka kwa watu 19 tofauti ambao inadaiwa walitoa kiasi tofauti cha fedha baada ya kuahidiwa watapata faida mara mbili hadi tatu ya fedha walizotoa.

Iliendelea kudaiwa kuwa mashitaka tisa ni ya utakatishaji yanayomkabili mshitakiwa Mkondya pekee.

Anadaiwa kati ya Januari Mosi 2020 na Desemba Mosi 2023, akiwa kama mkurugenzi wa kampuni hiyo, alijipatia viwanja tisa kitalu namba AB eneo la Idunda mkoani Njombe huku akijua viwanja hivyo ni mazalia ya makosa tangulizi ya upatu.

 

 

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button