Usafiri wa uhakika ni chachu biashara saa 24

MKOA wa Dar es Salaam unatarajiwa kuzindua ufanyaji wa biashara kwa saa 24 wiki ijayo.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alinukuliwa jana akisema utaratibu huu unategemewa kuongeza uchumi kutokana na kuongezeka kwa wigo wa biashara na ukusanyaji kodi.

Alisema maeneo yatakayoanza kufanya biashara saa 24 ni Kariakoo, Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli, Tandika,
Mbagala, Bunju, Manzese na Mwenge.

Chalamila amesema ili kufanikisha jambo hili la biashara kwa saa 24, wameanza kukaa na kuzungumza na wadau mbalimbali wakiwemo wa usafirishaji ili pia, waanze kutoa huduma kwa saa hizo.

Tunaunga mkono lengo hili la kuhakikisha kunakuwapo usafiri wa uhakika kwa saa 24 kuyafikia maeneo yaliyoainishwa.

Usafiri wa uhakika unamaanisha kuwa na njia za usafiri ambazo ni salama, za uhakika na zinazopatikana kwa urahisi saa zote za usiku na mchana.

Hili linahusu usafirishaji wa abiria kwa daladala, mabasi yaendayo haraka (mwendokasi), bajaji na hata pikipiki.

Usafiri wa uhakika utawezesha wateja na wafanyabiashara kusafiri kwa urahisi kwenda na kutoka maeneo ya biashara wakati wowote.

Hii ni muhimu kwa biashara zinazofanya kazi usiku, kwani itawavutia wateja wanaotafuta huduma au bidhaa wakati huo.

Kuwapo usafiri wa uhakika kutawezesha wafanyabiashara kusafirisha bidhaa na huduma zao kwa urahisi wakati wowote hatua itakayopunguza gharama, itawaongezea faida na hivyo kuongeza ufanisi wa biashara zao.

Tunatambua kwamba biashara ya saa 24 itaongeza mzunguko wa fedha na shughuli za kiuchumi kwa ujumla. Kwa hiyo ni muhimu kuwapo usafiri wa uhakika kuhakikisha watu wanafika kushiriki katika shughuli hizi za kiuchumi.

Kukiwapo daladala na mabasi ya mwendokasi hususani katika maeneo ya Kariakoo, ni wazi kutawezesha watu kufanya kazi wakati wowote na hivyo kutoa fursa zaidi za ajira kwa shughuli mbalimbali hususani za huduma.

Kwa kuwa Chalamila amesema wameanza kukaa na kuzungumza na wadau wakiwemo wa usafirishaji ili pia, waanze kutoa huduma kwa saa 24 ni matumaini mazungumzo haya yatazaa matunda.

Matunda yanayotegemewa ni ya serikali na wadau kujikita katika kuboresha usafiri wa umma na wa kibinafsi ili kuhakikisha kuwa usafiri wa uhakika unapatikana kwa wote.

Tunapozungumzia maeneo ya katikati ya Dar es Salaam hususani Kariakoo, mdau mkubwa zaidi anayetegemewa kukidhi haja hii ni Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) yenye jukumu kuu la kuendesha mfumo wa usafiri wa mabasi yaendayo haraka.

Mdau mwingine muhimu katika kuwezesha kuwapo usafiri wa uhakika usiku ni pamoja na Kikosi cha Usalama
Barabarani ambacho tunaamini mamlaka zinazohusika zitajipanga kuhakikisha usafirishaji unazingatia usalama barabarani.

Ni mategemeo yetu kwamba mazungumzo na wadau yataunga mkono biashara ya usiku kwa kuwapo usafiri wa uhakika na salama.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button