USAID yaipiga ‘jeki’ shule ya wasichana Sega

MOROGORO: Shirika la Marekani la USAID kupitia idara yake ya American Schools and Hospitals Abroad (ASHA) limetangaza ufadhili wa mradi wa ujenzi wa shule ya Sekondari ya Wasichana Sega iliyopo Mkundi, Kata ya Kihonda, Manispaa ya Morogoro.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo, Alhamisi na na Mkurugenzi shirika la SEGA na Meneja wa Shule ya Sekondari Sega, Laina Mwandoloma,  mradi huo umelenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kukuza maendeleo ya elimu kwa wanafunzi na jamii inayowazunguka.

“Mradi huu umeleta mwangaza kwa shule ya wasichana ya Sega, ambayo kwa sasa inahudumia wanafunzi 280 wenye vipaji ambao vinginevyo walikua kwenye hatari ya kutokuendelea na masomo au kutokupata elimu bora, kwa kuwapatia elimu bora sana pamoja na fursa mbalimbali zitakazowawezesha kufikia malengo yao.

“Ujenzi unalenga kuongeza miundombinu ya kisasa, ikiwa ni pamoja na bweni litakalobeba wasichana 48, maabara ya biolojia ambayo imekua ni hitaji la muda mrefu la shule hiyo na ina lengo la kuboresha ufundishaji kwa vitendo, uzio wa shule, karakana na kibanda cha mlinzi,” ameeleza.

Ameongeza kuwa ujenzi huu utaboresha mazingira ya kujifunzia na kuhakikisha usalama wa wanafunzi halikadhalika kuipa nafasi shule kuongeza na kuhudumia wanafunzi wengi zaidi na kuimarisha usalama kwa wanafunzi wa kike.

Mkurugenzi huo amesema kuwa shule imezungukwa na makazi ya watu, hivyo inahitaji mazingira yenye amani na utulivu ya kusomea ili kuzuia vishawishi vya wanafunzi kutoka nje ya shule.

Mradi utapanua wigo wa shule kwa kutoa mafunzo ya vitendo katika muziki, ufugaji kuku, ushonaji, na kilimo cha mbogamboga.

“Hii inatarajiwa kuwa na manufaa makubwa kwa wanafunzi na jamii ya SEGA kwa ujumla, ikilenga kutoa wahitimu wenye elimu ya stadi kazi ili waweze kufanikiwa na kuwa chachu ya mabadiliko chanya katika familia na jamii zao,” ameongeza.

Mradi huu unalenga kudumisha uhusiano wa kirafiki kati ya Tanzania na Marekani kwa kukuza misingi muhimu ya usawa wa kijinsia, uvumbuzi katika teknolojia, na ubunifu katika mbinu za kufundishia na kujifunza.

Pia, mradi unajikita katika ujenzi endelevu unaolenga utunzaji wa mazingira na kuzingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu, ambayo ni

misingi inayothaminiwa na jamii ya Marekani na inayopewa kipaumbele na Serikali ya Tanzania.

Shirika la Naturing Minds, lenye makao yake Marekani ambalo ndio mdhamini mkuu wa shule ya sekondari ya Sega, limepokea fedha zenye thamani ya dola za Kimarekani 476,000 kutoka kwa idara ya American Schools and Hospitals Abroad (ASHA) kwa lengo la kuboresha miundombinu ya Shule ya Sega.

Utekelezaji wa mradi huu unategemewa kuwa wa miaka minne na umeanza rasmi mwezi Oktoba, 2023 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba 2027.

“Tunawashukuru wadau wote waliochangia katika kufanikisha mradi huu na tunaendelea kuwakaribisha kushirikiana nasi katika juhudi zetu za kuboresha elimu nchini Tanzania,” amehitimisha.

Habari Zifananazo

Back to top button