Usajili laini za simu waongezeka 41% mikoa minne

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema ongezeko la minara ya mawasiliano ya simu za mkononi na mitambo ya kurushia mawimbi vimewezesha laini zinazotumika nchini kuongezeka kwa asilimia 35 ndani ya miezi 18.
Ripoti ya TCRA kuhusu hali ya mawasiliano nchini kati ya Januari na Machi mwaka huu inaonesha usajili wa laini za simu uliongezeka kwa asilimia 41 mikoa ya Kagera, Kigoma, Tabora na Tanga kati ya Septemba 2023 na Machi mwaka huu.
TCRA imeeleza kuwa hadi Machi, mwaka huu kulikuwa na minara 9,278 Tanzania kulinganisha na 8,551 iliyokuwepo Juni, mwaka jana hivyo kuna ongezeko la asilimia 8.5.
Serikali inakamilisha ujenzi wa minara ya mawasiliano ya simu 758 na kuboresha mingine 300 nchini kote ili iwezesha utoaji huduma kwa teknolojia ya uzao wa tatu, wa nne na wa tano wa mawasiliano ya simu kwa vifaa vya mkononi (3G, 4G na 5G).
Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) unasimamia mradi wa ujenzi na uboreshaji minara uliozinduliwa Mei 13, 2023 na Rais Samia Suluhu Hassan.
Serikali ya Tanzania pia imejenga minara 42 Unguja na Pemba.
Ripoti iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Jabiri Bakari ilieleza kuwa laini 67,024,338 zilikuwa zimesajiliwa nchini kote hadi Septemba 2023 na hadi Machi mwaka huu zimesajiliwa laini 90,298,941.
Dk Bakari alisema kuna ongezeko la laini kati ya Septemba 2023 na Machi mwaka huu kwenye mikoa hiyo minne na idadi kwenye mabano Kagera (1,577,159 hadi 2,224,115), Kigoma (kutoka 1,279,021 mpaka 1,803,679), Tabora (kutoka 3,099,517 kufikia 4,371,032) na Tanga kutoka 2,365,189 hadi 3,335,396.
Alisema mikoa hiyo pia ni miongoni mwa mikoa 12 yenye idadi kubwa ya mitambo inayowezesha mawasiliano ya 4G.
TCRA ilieleza kuwa uzao wa tano (5G) wa teknolojia ya mawasiliano kwa vifaa vya mkononi ilikuwa imeenea miongoni kwa watu kwa asilimia 23 na kijiografia nchini kwa asilimia 3.6 kufikia Machi mwaka huu.
Dk Bakari alisema mikoa yote sasa ina angalau mnara mmoja wenye mitambo ya 5G. Mikoa iliyokuwa haina hadi Juni mwaka jana ni Mtwara, Lindi, Kaskazini Pemba na Katavi.
Mikoa 10 inayoongoza kwa mitambo na idadi kwenye mabano ni Dar es Salaam (633), Mjini Magharibi Zanzibar (60), Dodoma (46), Mwanza (41), Arusha (34), Mbeya (16), Songwe (13) Morogoro (9), Pwani (9) na Kilimanjaro (8).
Teknolojia ya 5G iliingia Tanzania Septemba 2022 na ina ufanisi zaidi na inawezesha mifumo na programu tumizi zinazohitaji kasi kubwa ya data mitandaoni na ambayo inaunganisha na kuwezesha kutumika vifaa vingi kwa mara moja.
Hadi Machi mwaka huu teknolojia ya uzao wa pili (2G) imeenea kwa asilimia 98.4 ya wananchi, 3G asilimia 92.2, 4G asilimia 90.7 na 5G asilimia 23.



