Ushahidi pasua kichwa kesi za ukatili Bukombe

OFISI ya Dawati la Jinsia katika Kituo cha Polisi Bukombe imeeleza kuwa bado kuna changamoto kubwa ya ndugu, jamaa na marafiki kufika mahakamani kutoa ushahidi pale watuhumiwa wa ukatili wa kijinsia wanapokamatwa.
Ofisa wa Dawati la Jinsia wilayani humo, Eliwaja Nelson alisema hayo wakati akizungumza na wachimbaji wadogo kijiji cha Katente Namba moja, kata ya Katente ikiwa ni sehemu ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC).
Amesema mara nyingi matukio ya ukatili wa kijinsia yanapotokea na kuripotiwa dawati la jinsia kwa ushirikiano na jeshi la polisi wanapofanikisha kumtia hatiani mtuhumiwa tatizo kubwa imekuwa ni kupata ushahidi.
“Tukio la ukatili likiripotiwa mnashindwa kutoa ushirikiano kesi inapokuwa mahakamani, ili kufikia muafaka mzuri, tunawaita kuja kutoa ushahidi hamjitokezi kabisaa.
“Kwa hiyo tunakuwa hatujamtendea haki yule ambaye amefanyiwa ukatili. Tunawaita kuja kutoa ushahidi ili yule aliyefanyiwa ukatili apate haki zake na yule aliyefanya ukatili achukuliwe hatua za kisheria.
“Mnatuangusha pale ambapo mnashindwa kuja kutoa ushahidi mahakamani ili yule aliyefanyiwa ukatili apate haki zake, kwa hiyo nawaomba pale unapopata wito wa kuja kutoa ushahidi mahakamani ufike”, amesema Eliwaja.
Amesema dawati la jinsia Bukombe wamebaini pia baadhi ya wazazi wanahusika kuwalaghai watoto wao waliobakwa kutotoa ushahidi ili waolewe ama kulipwa pesa kama fidia kwa mtu aliyetenda ukatili huo.
Eliwaja ametaja aina kuu nne za ukatili wa kijinsia ambazo zimeshamiri na kuathiri jamii wilayani humo ambazo ni ukatili wa kimwili, ukatili wa kingono, ukatili wa kisaikolojia ipamoja na ukatili wa kiuchumi.
Amesema sababu kuu zinazochangia matukio ya ukatili wilayani humo ni ukosefu wa elimu, mila na desturi potofu pamoja na uelewa duni wa sheria na haki za binadamu.
“Kwa mfano mchimbaji unaambiwa utuletee kiungo cha mtu mwenye ulemavu wa ngozi, unaenda unamutafuta mtu mwenye ulemavu wa ngozi unamkata kiungo ili upeleke kwa mganga”, amesema.
Amesema uchunguzi umebaini kuwa ukatili unafanyika sehemu mbalimbali ikiwemo mgodini, maofisini na majumbani ambapo waathirika wakubwa wamekuwa ni watoto, wanawake na watu wenye ulemavu.
Eliwaja ametaja sehemu sahihi za kuripoti matukio ya ukatili ni kituo cha polisi, ustawi wa jamii, dawati la jinsia, hospitalini, shuleni pamoja na ofisi za viongozi wa serikali za mitaa ikiwemo wenyeviti wa vitongoji na vijiji.



