Ushirikiano NIT, mabibo waboresha huduma kwa wananchi

DAR ES SALAAM: Ushirikiano kati ya taasisi za elimu na jamii zinazozunguka umeendelea kuonesha mchango wake katika kutatua changamoto za kijamii, baada ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kujenga na kukabidhi ofisi mpya ya Serikali ya Mtaa wa Mabibo, Wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam.
Ofisi hiyo inatarajiwa kuboresha mazingira ya utendaji kazi wa viongozi wa Serikali ya Mtaa na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kiutawala kwa wananchi, ambao awali walikabiliwa na changamoto za miundombinu ya ofisi.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Wakili Albert Msando, amesema mradi huo ni mfano wa namna taasisi za elimu zinavyoweza kutumia nafasi na rasilimali zake kushiriki katika kutatua changamoto zinazozikabili jamii.
Amesema uwepo wa ofisi bora ni sehemu muhimu ya kuimarisha utendaji wa Serikali za Mitaa, kwa kuwa viongozi wanahitaji mazingira yanayowawezesha kuwahudumia wananchi na kushughulikia changamoto zinazojitokeza katika maeneo yao.
“Naupongeza uongozi wa NIT chini ya Mkuu wa Chuo hicho, Mhandisi Dkt. Prosper Mgaya, kwa ubunifu na ushirikiano uliooneshwa katika kutekeleza mradi huu. Hatua hii ni mfano mzuri wa ushirikiano kati ya taasisi za elimu na jamii inayozunguka,” amesema Msando.

Amehimiza madiwani, maafisa tarafa na wenyeviti wa Serikali za Mitaa kuweka kipaumbele katika kuboresha miundombinu ya ofisi, akieleza kuwa viongozi wanapaswa kuwa na maeneo rasmi yanayopatikana kwa urahisi ili wananchi waweze kuwasilisha changamoto na kupata msaada kwa wakati.
Amesema changamoto zinazohitaji ushiriki wa viongozi wa mitaa ni pamoja na upatikanaji wa maji, mafuriko, usafi wa mazingira na masuala mengine yanayogusa maisha ya kila siku ya wananchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha NIT, Mhandisi Dkt. Prosper Mgaya, amesema ujenzi wa ofisi hiyo umetokana na dhamira ya chuo kuimarisha uhusiano na jamii inayokizunguka, ikiwemo kuchangia upatikanaji wa huduma muhimu.
Amesema uamuzi wa kujenga ofisi hiyo ulizingatia mahitaji ya wananchi wa Mabibo na idadi kubwa ya wanafunzi wa NIT wanaohitaji huduma za Serikali ya Mtaa, hivyo umuhimu wa kuwa na miundombinu inayorahisisha upatikanaji wa huduma hizo.
Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya NIT na Serikali ya Mtaa wa Mabibo umekuwa na mchango katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wanafunzi wa chuo hicho na jamii kwa ujumla.
Ofisi hiyo ina vyumba viwili vya ofisi, chumba cha kuhifadhia vifaa, choo na chumba kimoja cha biashara. Pia imeunganishwa na huduma za maji safi na umeme ili kuwezesha shughuli za kiutawala kufanyika katika mazingira yanayofaa.
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mabibo, Nasib Mangushi, amesema ujenzi huo umetatua changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji wa mazingira bora ya kufanyia kazi, iliyokuwa ikiikabili Serikali ya Mtaa.
Amesema juhudi za kupata ofisi hiyo zilianza Oktoba 2019, baada ya viongozi wa mtaa kuwasilisha ombi kwa NIT wakieleza changamoto walizokuwa wakikabiliana nazo na kuomba chuo hicho kishiriki katika ujenzi wa ofisi mpya.
Amesema NIT ilipokea ombi hilo na kulifanyia kazi, hatua iliyowezesha kukamilika kwa mradi huo na kukabidhiwa rasmi kwa Serikali ya Mtaa.
“Kwa kweli tunakishukuru Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kwa kuwa wadau wazuri wa maendeleo. Tulipokumbana na changamoto za ofisi Oktoba 29, tuliwapelekea barua kuwaomba watuunge mkono katika ujenzi, na leo hii tumekabidhiwa rasmi ofisi ya kisasa,” amesema.
Ameeleza kuwa ofisi hiyo itaimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuweka mazingira bora zaidi kwa viongozi kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Ujenzi wa ofisi hiyo unaonesha umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi za elimu na Serikali za Mitaa katika kukabiliana na changamoto za kijamii, hususan kuboresha miundombinu inayowezesha wananchi kupata huduma karibu na maeneo wanayoishi.



