Usiseme Simba! Sema mwakilishi wetu

DAR ES SALAAM; SIMBA wameanza kutamba bwana! Leo walijana pale Viwanja vya Mwembe Yanga, Temeke, Dar es Salaam kufuatilia kwenye televisheni mchezo wa mwisho hatua ya makundi kati ya timu hiyo na CS Constantine ya Algeria uliokuwa unachezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

“Sisi ndiyo wawakilishi pekee wa Tanzania tuliobaki kimataifa. Hivi sasa hutakiwi kuuliza vipi kuhusu Simba, bali useme vipi kuhusu wawakilishi wetu kimataifa?” Hiyo ni kauli iliyokuwa ikizungumzwa na Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally akiwa kwenye viwanja hivyo na mashabiki wengine.

Mashabiki nao waliibeba kauli hiyo wakitamba wao ndiyo pekee waliobaki hivi sasa wakipeperusha bendera ya Tanzania baada ya timu nyingine za Tanzania kutupwa nje.

Advertisement

Tanzania ilikuwa na timu sita michuano ya mwaka huu, ambapo tatu zilikuwa Ligi ya Mabingwa ambazo ni Yanga, Azam na JKU, wakati tatu za Kombe la Shirikisho ni Simba, Coastal na Uhamiaji.

Katike mchezo wa leo ambao haukuruhusiwa mashabiki, Simba imeibuka na ushindi wa mabao 2-0, wafungaji wakiwa Kibu Dennis na Leonel Ateba.

Matokeo hayo yameifanya Simba ambayo tayari ilishafuzu robo fainali, imalize mechi za makundi ikiwa kinara wa Kundi A kwa pointi 13, ikifuatiwa na CS Constantine yenye pointi 12, Bravos yenye pointi 7 na CS Sfaxien yenye pointi tatu ilizopata leo baada ya kuifunga Bravos mabao 4-0. CS Constantine pia imefuzu robo fainali.