Utafiti kusaidia mapambano ya njaa ifikapo 2030

Serikali imepanga kufanya utafiti wa kina katika sekta za kilimo, uvuvi, na ufugaji ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa yanayolenga kumaliza njaa ifikapo mwaka 2030.

Taarifa hiyo ilitolewa na Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi, Anna Makinda, wakati akifunga mafunzo ya siku 14 kwa wadadisi na wasimamizi 178 wa kilimo kwa mwaka wa 2023/2024, yaliyofanyika katika Chuo cha Afya ya Msingi, mjini Iringa.

Makinda amesema jukumu kubwa la wadadisi na wasimamizi hao litakuwa ni kukusanya na kuchambua takwimu sahihi kuhusu uzalishaji katika kilimo, ufugaji, na uvuvi katika jamii.

Advertisement

Takwimu hizo alisema zitasaidia kuongeza uzalishaji na kuwezesha nchi kufikia viwango vya kimataifa vya mipango ya uzalishaji.

Amesisitiza umuhimu wa takwimu sahihi kwa maendeleo ya taifa, akisema, “Roho na uhai wa nchi unategemea takwimu sahihi. Takwimu hizi zitawasaidia wakulima kujua ni kiasi gani cha mbolea kinahitajika kwa shamba la ukubwa fulani na hivyo kuweza kubashiri mavuno.”

Aidha, Makinda amesema baada ya kukamilika kwa utafiti huo, jamii zitaweza kufaidika na miradi ya maendeleo iliyopangwa kwa misingi ya mahitaji halisi yaliyobainishwa kupitia takwimu.

“Miradi hiyo itapewa kipaumbele kulingana na maeneo yenye uhitaji mkubwa zaidi,” amesema.

Mtakwimu Mkuu kutoka Zanzibar, Kasimu Salim Ally, amesema mafunzo kama hayo yanaendelea pia visiwani Zanzibar na akahimiza washiriki kutimiza wajibu wao ili kufanikisha malengo ya utafiti huo muhimu.

Awali, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Albina Chuwa, amesema maandalizi ya takwimu za kilimo, uvuvi, na ufugaji yatasaidia kuweka sera bora za kukuza sekta hizo.

“Utafiti huu utaiwezesha serikali kupima hatua zilizofikiwa katika mapambano dhidi ya njaa kabla ya mwaka 2030,” amesema.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo walionesha matumaini makubwa, wakisema kuwa kupitia takwimu watakazokusanya, wataweza kusaidia kukuza sekta ya kilimo, uvuvi, na ufugaji kwa kuandaa takwimu zitakazowezesha mipango ya maendeleo katika maeneo yao.