‘Vibanda umiza tishio ukatili wa kingono’

DAR ES SALAAM; UTAFITI umebaini kuwa maeneo yanayooneshwa mpira au picha za video mitaani maarufu kama vibanda umiza, yamekuwa yakitumika katika ukatili wa kingono kwa watoto wa kiume.

Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu ( DUCE) cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Robert Mushema amesema hayo alipozungumzia utafiti uliofanywa wa ukatili dhidi ya watoto wa kiume.

Isome pia:https://habarileo.co.tz/marufuku-watoto-kupelekwa-vibanda-vya-video/

Advertisement

Amesema katika utafiti walioufanya mikoa minne, umeonesha kuwa watoto wa kiume wamekuwa wakifanyiwa ukatili katika maeneo ya vibanda umiza na kueleza kuwa utafiti huo wamebaini ukatili unaoongoza wanaofanyiwa watoto hao ni wa kingono ukifuatiwa wa kihisia.

“Kuna siri kubwa zinazotokea ngazi ya familia na jamii kuhusu ndugu wa karibu kuwafanyia ukatili wa kingono watoto wa ndugu zao,” amesema na kuongeza kuwa mikoa iliyofanyiwa utafiti huo ni Dar es Salaam, Mtwara, Songwe na Kigoma.

Amesema kinachosababisha matukio hayo yasiripotiwe ni watu wengi kutoelewa maana ya ukatili, kukosekana kwa ushahidi, mchakato wa uendeshaji wa kesi hizo kuwa mrefu pamoja na tamaduni za eneo husika.

Kutokana na hali hiyo wameshauri marekebisho katika mfumo wa kuripoti kesi, kuondoa mchakato mrefu wa kushughulikia kesi hizo, kuwawezasha maofisa ustawi wa jamii pamoja na kuanzishwa dawati la jinsia ngazi ya kata.