Uteuzi wagombea urais, ubunge, udiwani leo

UREJESHAJI wa fomu na uteuzi wa wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais unafanyika leo katika ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) zilizopo eneo la Njedengwa, Dodoma.
Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari kuhusu uteuzi huo, ilisema tume itakamilisha mchakato huo leo kuanzia saa 1:30 asubuhi hadi saa 10:00 alasiri.
Mchakato huo unafanyika kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 50 na 62 vya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, vikisomwa pamoja na kanuni ya 23 na 26 za Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za Mwaka 2025.
Uteuzi wa wagombea wa Ubunge kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Madiwani kwa Tanzania Bara unafanywa na wasimamizi wa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi katika ngazi ya jimbo kwa wagombea ubunge na ngazi ya kata kwa wagombea udiwani.