UVCCM: Amani ya Tanzania ni faraja kwa majirani

DAR ES SALAAM: MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Mohamed Kawaida, amesema Tanzania ikiwa na amani ni faraja kwa nchi jirani, hasa zile zinazotegemea Bandari ya Dar es Salaam kwa biashara.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Kawaida amesema kuwa kitendo cha baadhi y vijana kushiriki vitendo vya vurugu kwenye baadhi ya maeneo Oktoba 29, 2025, wakati wa Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani i kinyume cha maadili, sheria, mila na taratibu za jamii mbalimbali.
Amesema vurugu zimeathiri biashara za kikanda kwa nchi jirani kama Malawi, Zambia, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Uganda, ambazo hutegemea Bandari ya Dar es Salaam kwa usafirishaji wa bidhaa.
“Vijana wenzangu, mnapofanya vurugu hapa nyumbani, maumivu yake hayabaki Tanzania pekee, yanawafikia pia vijana wa nchi jirani wanaotegemea amani yetu kwa ustawi wa biashara,” amesema Kawaida.
Amesema kuwa baadhi ya watu walioratibu vurugu hizo hawapo nchini, na wengi wao si raia wa Tanzania bali waliwahamasisha vijana kupitia mitandao ya kijamii kufanya fujo ,huku wao wakistarehe nje ya nchi.
“Vurugu hizi si demokrasia, ni uhalifu. Uhuru wa kuandamana haumaanishi uhuru wa kuharibu mali au kuhatarisha maisha ya wengine,” amesema na kuwasihi vijana kushikamana kuilinda amani ya Tanzania.



